Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usipomsaidia mhamiaji leo, unaijuaje kesho yako?-Asya Omar Mwilima

Asya Omar Mwilima ni mhamiaji kutoka Zanzibar Tanzania ambaye alihamia nchini Marekani takribani miaka 20.
UN News/Anold Kayanda
Asya Omar Mwilima ni mhamiaji kutoka Zanzibar Tanzania ambaye alihamia nchini Marekani takribani miaka 20.

Usipomsaidia mhamiaji leo, unaijuaje kesho yako?-Asya Omar Mwilima

Wahamiaji na Wakimbizi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na viongozi wengine wa juu wa Umoja wa Mataifa, wakitoa wito kwa dunia kuhakikishia ulinzi wa haki za binadamu kwa wahamiaji. Asya Omar Mwilima ni mhamiaji kutoka Zanzibar Tanzania ambaye alihamia nchini Marekani takribani miaka 20 iliyopita na anakubaliana na wito wa Umoja wa Mataifa.

Asya Omar Mwilima ni mhamiaji kutoka Zanzibar Tanzania ambaye alihamia nchini Marekani takribani miaka 20 iliyopita. Je, amepokeaje ujumbe wa mwaka huu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa?“Napokea ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa vizuri kwasababu mhamiaji  ni binadamu kama binadamu mwingine. Yule aliyezaliwa pale pale na yule aliyehamia, wote wana haki sawa, wote wana mahitaji sawa, wote maisha yao yana thamani sawasawa.  Kwa hiyo siyo kwasababu ni mhamiaji  maisha yangu yawe kwenye hatari. Mimi kama binadamu nina haki ya maisha yangu kuthaminiwa, kulindwa. Kwa hivyo ninakubaliana na Katibu Mkuu kwamba kila uhamiaji popote alipo ana haki ya  kupewa ulinzi na  ana haki ya kuthaminiwa, ana haki ya  kuheshimiwa.”

Wahamiaji na wakimbizi kutoka nchi tofauti wakiwasili kwa treni maalumu katika mji wa Berlin Ujerumani
UNICEF/Ashley Gilbertson VII
Wahamiaji na wakimbizi kutoka nchi tofauti wakiwasili kwa treni maalumu katika mji wa Berlin Ujerumani

 

Na je anahisi vipi anaposikia kuwa  kuna nchi ambazo zinawazuia wahamiaji, Asya Omar Mwilima anasema,“Mimi ninajisikia vibaya kwasababu mpaka mtu aamue kuhamia nchini kwako kuna vitu vingi ambavyo   vimemsababishia. Mwingine anahamia kwa furaha tu na mapenzi yake. Mwingine ni mazingira tu yanamlazimu kwamba   lazima nihame hapa yaani kwa ajili ya usalama wangu au usalama  wa  familia yangu  inabidi niondoke hapa niende sehemu nyingine nikaanzishe maisha. Halafu pia tujue maisha yanabadilika. Leo yule ametaka kuhamia  kwako unamkataza hujui kesho na keshokutwa maisha yatabadilika vipi. Kesho na keshokutwa kwako kunaweza kutokea kitu kibaya  ukakimbilia kulekule ambako  uliwakataza wenzako wasije kwako  lakini huwezi kujua nani atakusaidia hapa duniani.”

Ni nyakati za asubuhi katika kituo cha Qanfoodah wanakoshikiliwa wahamiaji na  wanaume hawa waafrika wanasubiri kuitwa majina yao ili kuthibitisha uwepo wao.
OCHA/Giles Clarke
Ni nyakati za asubuhi katika kituo cha Qanfoodah wanakoshikiliwa wahamiaji na wanaume hawa waafrika wanasubiri kuitwa majina yao ili kuthibitisha uwepo wao.

 

Bi Mwilima ana ushauri gani kwa watu hususani vijana wanaotaka kuhama katika nchi zao?“Muhimu awe na malengo, na pia usome mazingira ya kule unayokwenda na pia  usome   katika nchi unayokwenda kuna fursa za namna gani ambazo wewe kama mhamiaji unaweza ukanufaika nazo. Kwa hiyo kama kijana kuna fursa nyingi ambazo labda  nyumbani hazipo, kwa hiyo jua   ni namna gani na fursa za aina  gani na jinsi gani  utaweza kupata nafasi ya kupata zile fursa. Muhimu popote  unakokwenda zingatia kanuni na sheria za nchi, usijiingize kwenye mambo ambayo unajua haya yatanitia kwenye matatizo haya.”