Wahamiaji wote wana haki ya ulinzi sawa wa haki zao zote za kibinadamu-UN

Picha ya maktaba ikionesha wahamiaji na wakimbizi wakisubiri kupandisha mizingo yao kwenye ndege tayari kwa kuhamishwa kutoka Tripoli Libya
IOM TRIPOLI
Picha ya maktaba ikionesha wahamiaji na wakimbizi wakisubiri kupandisha mizingo yao kwenye ndege tayari kwa kuhamishwa kutoka Tripoli Libya

Wahamiaji wote wana haki ya ulinzi sawa wa haki zao zote za kibinadamu-UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na viongozi wengine wa juu wa Umoja wa Mataifa, wametoa wito kwa dunia kuhakikishia ulinzi wa haki za binadamu kwa wahamiaji. 

Bwana Antonio Guterres katika wito huo wakati wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya uhamiaji ambayo huadhimishwa kila mwaka  tarehe 18 mwezi Desemba amesema ulimwengu unaitumia siku hii kukuza uelewa juu ya uhamiaji na wahamiaji, na kwamba,“wahamiaji wote wanastahili ulinzi sawa wa haki zao za binadamu. Katika siku hii ya kimataifa, ninawasihi viongozi wote kila mahali kudumisha mkataba wa kimataifa kuhusu uhamiaji, ili uhamiaji uweze kuwafaa watu wote.”

Aidha Katibu Mkuu amesema wahamiaji ni washirika muhimu wa jamii, wanachangia katika uelewa wa pamoja na maendeleo endelevu katika jamii za asili walikotoka na waliko sasa,“Na mara nyingi tunashuhudia wahamiaji wanakabiliwa na ugumu usioelezeka kutokana na sera zilizowekwa kutokana na hofu zaidi kuliko ukweli.”

Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa, duniani, kuna wahamiaji zaidi ya milioni 270. Mwezi Desemba mwaka jana, nchi zilikubaliana katika mktaba kuhusu wahamiaji kwa upande wa usalama, uhamiaji uliopangwa na wa kawaida kufuatia miezi 18 ya mashauriano na majadiliano.

Kwa upande wake Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na wahamiaji, IOM, Antonio Vitorino amesema kuwa jamii wenyeji kote duniani zina utamaduni wa muda mrefu wa kuwaakaribisha wageni na kuongeza kuwa "Jamii zinazoendelea ni zile ambazo hukumbatia mabadiliko na kuendana nayo. Wahamiaji ni sehemu muhimu na inayokubalika ya mabadiliko hayo.”

Naye Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amesema, “ kila mtu anayehama ana sababu zake za kuacha nyumba makazi yake na familia yake na kila mmoja wa watu hawa ana uzooefu wa kipekee katika safari hiyo; hadithi zao binafsi za kuhama na mali zao.”

Yeye mwenyewe Bi Bachelet akiwa amezaliwa nchini Chile, amesema alikuwa na babu yake ambaye alihama Ufaransa na kuelekea katika nchi hyo ya Amerika ya Kusini ambako Bi Bachelet alizaliwa na kufikia kuwa rais wa nchi hiyo kwa vipindi viwili.