Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtengeneza muziki mmarekani aahamishia studio yake Beirut kuwarekodi wakimbizi wa Syria

Jiji la Beirut, Lebanon
World Bank/Dominic Chavez
Jiji la Beirut, Lebanon

Mtengeneza muziki mmarekani aahamishia studio yake Beirut kuwarekodi wakimbizi wa Syria

Wahamiaji na Wakimbizi

Mtengenezaji wa muziki, mmarekani Jay Denton, amesafiri hadi nchini Lebanon kuandaa Albamu ya muziki kwa kushirikiana na wakimbizi wa huko kwa kuwapatia nafasi ya kupaza sauti na kueleza uzoefu wao.

Ni Souzda Ammo, mkimbizi kutoka Syria akirekodi wimbo wake unaoeleza maumivu yake, anasema,“muziki ni maisha, ni lugha ambayo kwayo ninaweza kujieleza. Ninaweza kueleza maumivu yangu, furaha yangu, ninaweza kuzungumza kupitia muziki. Hiyo ndio lugha iliyoko karibu na mioyo ya watu.”

Souzda anaimba kwa ajili ya Afrin, mji wake wa nyumbani, kaskazini mwa Syria. Alijaribu kuishi ndani ya mazingira vita huko kwao nchini Syria,“nilifikia wakati ambao sikuweza kumudu kuona damu tena, kusikia mabomu, nilikuwa nafanya kazi hospital na nilikuwa naona haya kila siku. Nilikuwa pia najifunza muziki na sikuweza kuendelea na masomo yangu kwasababu ya vita.”

Hatimaye alikimbilia Lebanon, huko akakutana na mtengeneza muziki, Jay Denton kutoka Marekani, anasema“nilileta studio hapa kurekodi  muziki na wakimbizi wa Syria hapa Beirut.”

Akiwa ameshawishiwa na simulizi za wakimbizi, Jay alitaka kurekodi sauti zao, “Mara ya kwanza nilipokuwa ninaongea nao waliniambia moja ya vitu vigumu hapa kuhusu maisha ni kuwa wanajihisi kama hawana kauli.”

Jay ameshirikiana na wakimbizi 14 kwa ushirikiano na wasanii kadhaa wa Marekani, “baadhi ya nyimbo zinahusu hisia tu za ujumla kuhusu mathalani ilivyo kuwa mbali na nyumbani. Baadhi ya nyimbo zinahusu matumaini na kutafuta matumaini katikati mwa nyakati ngumu.”

Ndoto ya Souzda ni kuiimbia dunia na anasema ni kweli nchini mwake kuna vita lakini ana matumaini ya kuendelea kimuziki. 

Albamu itaachiwa katika kipindi hiki chaa mwisho wa mwaka.