Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nilichokiona Beirut sitosahau katu -Mkimbizi wa Syria

Mwanamke mmoja huko Beirut anatafuta mabaki nyumbani mwake baada ya mlipuko wa tarehe 4 Agosti kuporomosha nyumba yake.
© UNOCHA
Mwanamke mmoja huko Beirut anatafuta mabaki nyumbani mwake baada ya mlipuko wa tarehe 4 Agosti kuporomosha nyumba yake.

Nilichokiona Beirut sitosahau katu -Mkimbizi wa Syria

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Lebanon, wakimbizi kutoka Syria walionusurika katika mlipuko mkubwa wa tarehe 4 mwezi huu wa Agosti kwenye mji mkuu wa Lebanon, Beirut wamesimulia kile ambacho walishuhudia na kiwewe kilichowakumba katika tukio hilo lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 170 na wengine zaidi ya 6,500 wamejeruhiwa.

Miongoni mwa wakimbizi hao ni Aisha ambaye anasema kuwa yeye na watoto wake wawili, Zakarya na Yahya, walisikia kishindo cha mlio wakidhani ni ndege na walipochungulia dirishani kila kitu kilisambaratika. 

Aisha anasema kuwa, “kushuhudia mtoto wangu anavuja damu kichwani na sisi tunashindwa kuizuia, lilikuwa ni jambo gumu sana. Nami sikuwa na habari kuwa nilikuwa nimejeruhiwa.” 

Mkimbizi mwingine, Ahmed akisimulia tukio hilo anaeleza kuwa walisikia mlio. Niliwafuata. Walipofika katikati ya chumba, madirisha yote na vioo vikawaangukia. Kwa kweli siwezi kusimulia.” 

Milipuko hiyo miwili mikubwa ambayo ilikumba Beirut ilivunja madirisha na vioo ya nyumba ya wakimbizi hao na vifusi vya vioo, madirisha na matofali vikawafunika watoto hao wawili na mama yao. 

Mlipuko wa Beirut mnamo 4 Agosti 2020 ambao uliwaacha wengi bila makaazi
© UNOCHA
Mlipuko wa Beirut mnamo 4 Agosti 2020 ambao uliwaacha wengi bila makaazi

Aisha anaendelea kusimulia akisema kuwa, “ni kitu ambacho sijawahi kukihisi awali. Nilidhani nyumba yote imelipuka. Sikuweza kuona chochote. Vumbi lilijaa kila kona. Nilimsikia mume wangu akipaza sauti, Aisha! Mungu wangu, Mungu wangu! Yahya, Zakariya!” 

Familia hiyo kutoka Hassakah nchini Syria inasema kuwa machungu waliyopitia na kile walichoshuhudia kitasalia kwenye fikra na miili yao kwa muda mrefu.