Wanawake wawili waanzisha kituo cha elimu kwa watoto wakimbizi nchini Lebanon

5 Septemba 2019

Nchini Lebanon mashirika ya kiraia yanaitikia wito wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia watoto wakimbizi kuendelea na masomo hata baada ya kujikuta ukimbizini.

Katika viunga vya mji mkuu wa Lebanon, Beirut, kuna kituo kinachowapatia fursa ya elimu watoto wakimbizi kutoka Syria ambao awali walikuwa mitaani na wakitumikishwa.

Kituo hiki cha shirika lisilo la kiserikali liitwalo Borderless kimewakaribisha watoto wakimbizi 150 ili kuwasaidia kuendelea na masomo yao. Miongoni mwao ni Faheed ambaye kabla ya kuja hapa alitumikishwa saa 10 kwa siku akiwa na umri wa miaka 10 tu.

 (Sauti ya Fahed)

"Mwajiri wangu alikuwa akinipiga. Iwapo sikuweza kubeba mzigo ananipiga akinilazimisha kubeba.”

Hivi sasa, Fahed yuko salama na anaenda shule hii isiyo rasmi ya watoto wakimbizi mjini  Beirut na anasema anaifurahia hali hiyo, kwani anajifunza na kucheza na marafiki zake.

Ali ni mkimbizi kutoka Syria naye anasema hufika kituoni kusoma kiarabu, kiingereza na hisabati lakini anaendelea kufanya kazi,

(Sauti ya Ali)

"Shule ni muhimu zaidi kuliko kazi…Lakini sina budi kufanya kazi kuwasaidia wazazi wangu. ”

Randa Ajami kutoka Lebanon ni mwanzilishi mwenza wa kituo hiki.

 (Sauti ya Randa Ajami)

"Unawaondoa barabarani. Unawapa kitu ambacho wangependa kuwa nacho na ambacho wazazi wao wangependa kuwa nacho na hiyo ni elimu."

Kituo hiki  kinategemea michango lakini mara nyingi michango hiyo hutokea mara moja moja na shule inahitaji msaada endelevu ili kuendelea, la sivyo, watoto wengi wako hatarini kurudi mitaani, na kupoteza fursa yao ya kustawi na kuwa na ndoto ya maisha bora ya baadaye.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud