Katika viunga vya mji mkuu wa Mauritania, Nouakchott, bustani ya mapangaboi ya kuzalisha umeme kwa njia ya upepo  yanaonekana kwa mbali na ni jawabu sahihi katika kuwa na nishati rejelezi

Safari ya kuanzia UNFCCC hadi COP25:

UNDP Mauritania/Freya Morales
Katika viunga vya mji mkuu wa Mauritania, Nouakchott, bustani ya mapangaboi ya kuzalisha umeme kwa njia ya upepo yanaonekana kwa mbali na ni jawabu sahihi katika kuwa na nishati rejelezi

Safari ya kuanzia UNFCCC hadi COP25:

Tabianchi na mazingira

Mabadiliko ya tabianchi yanatokea. Joto duniani sasa hivi ni nyuzi joto 1.1 zaidi ya ilivyokuwa mwanzoni mwa mapinduzi ya viwanda, na tayari linaleta madhara makubwa kwa ulimwengu, na kwa maisha ya watu. Ikiwa kiwango cha sasa kitazidi, basi kiwango cha joto duniani kinaweza kuongezeka kwa nyuzi joto 3.4 hadi 3.9 kwenye kipimo cha selsiyasi katika karne hii, kiwango ambacho kinaweza kusababisha madhara makubwa zaidi na yenye uharibifu kwa tabianchi.

Hilo ndilo onyo kali kutoka kwa jamii ya kimataifa kabla ya kikao cha ngazi ya juu cha mkutano wa 25 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP25, ambao unaendelea katika mji mkuu wa Hispania, Madrid tangu Desemba 2 mwaka huu. Kwa hiyo basi, miezi miwili tu baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kufanya mkutano mkubwa wa Hatua kwa tabianchi katika Makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, nini kinaweza kutarajiwa kutoka kwa COP25?

1. Tofauti kati ya Mkutano wa Hatua za mabadiliko ya tabianchi tuliokuwa nao mjini New York na COP25 ni ipi?

Mkutano wa Hatua za mabadiliko ya tabianchi mnamo Septemba 2019 ulikuwa hatua ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuzingatia umakini wa jamii ya kimataifa kwa dharura ya tabianchi na kuharakisha hatua za kugeuza mabadiliko ya tabianchi. 

Mkutano wa COP25 unaofanyika mjini Madrid baada ya kuhamishwa kutoka Chile kwa sababu za machafuko huko, ndio mkutano halisi wa wanachama wa mkataba wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC, ambao sasa una jukumu la kuhakikisha kwamba mkataba huo ambao sasa unajulikana kama mataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2015, unatekelezwa.

2.  Kwa nini huu umakini wote wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi?

UNFCCC
UNFCCC

Kuna ushahidi zaidi wa madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi, haswa katika vipindi vya hali ya hewa vilivyokithiri, na madhara haya yanazidi. Sayansi inaonyesha kwamba uzalishaji wa hewa ya ukaa bado unaongezeka, haupunguki.Kulingana na chapisho la shirika la hali ya hewa duniani, WMO kuhusu utoaji wa hewa chafuzi, viwango vya gesi chafuzi angani vimefikia rekodi nyingine mpya ya juu. Hali hii inayoendelea kwa muda mrefu inamaanisha kwamba vizazi vijavyo vitakabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na ongezeko wa joto, hali ya hewa kali zaidi, uhaba wa maji, kuongezeka kwa kiwango cha maji ya bahari na kuvurugwa kwa mazingira ya baharini na bayonuai.

 

Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa,UNEFP, kupitia ripoti yake ya mwaka huu kuhusu utoaji wa hewa chafuzi limeonya kuwa kupunguza utoaji wahewa chafuzi kwa asilimia 7.6 kila mwaka kuanzia mwaka 2020 hadi 2030 ni muhimu ili kufikia lengo la kimataifa la kuhakikisha kiwango cha ongezeko la joto hakivuki nyuzi joto 1.5 ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda. Wanasayansi wanakubali kwamba hilo ni lengo la juu mno ilhali fursa za kulifikia ni finyu.

3. Hivyo, mkutano wa tabianchi wa Septemba ulifanikisha nini?

Mtizamo wa Baraza Kuu wakati wa ufunguzi wa kongamano la hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi mwaka 2019. (Septemba 23, 2019)
UN Photo/Loey Felipe

Mkutano huo ulinyoosha njia tunapokaribia mwaka 2020 uliowekwa na Mkataba wa Paris, kulenga umakini wa ulimwengu kuhusu dharura ya tabianchi na hitaji la dharura la kuongeza hatua. Na viongozi, kutoka sekta na nchi nyingi, walipiga hatua.

Zaidi ya nchi 70 ziliazimia kuhakikisha zinaondokana kabisa na uzalishaji wa hewa ya ukaa ifikapo mwaka 2050 hata kama wachafuzi wa kubwa au wazalishaji wakubwa wa hewa hiyo watakuwa bado kufanya hivyo. Zaidi ya miji 100 imechukua hatua hizo,  ikiwemo majiji makubwa zaidi duniani.

Nchi za visiwa vidogo kwa pamoja, zimejitolea kumaliza uzalishaji wa hewa chafuzi na kuhamia kwenye kutumia kwa asilimia 100 nishati mbadala fikapo mwaka 2030. Nchi kuanzia Pakistan hadi Guatemala, Colombia hadi Nigeria, New Zealand hadi Barbados ziliahidi kupanda miti zaidi ya bilioni 11.

Zaidi ya viongozi 100 wa sekta binafsi wamejitolea kuharakisha uchumi rafiki kwa mazingira. Kundi la wamiliki wakubwa wa rasilimali duniani likidhibiti dola trilioni 2, liliahidi kuhamia uwekezaji usiotoa hewa chafuzi ifikapo 2050. Hii ni pamoja na wito wa hivi karibuni wa wasimamizi wa mali wanaowakilisha karibu nusu ya mitaji duniani, sawa na dola trilioni 34, kwa viongozi wa ulimwengu kutoza gharama ya juu kwenye hewa ya ukaa na kuondoa ruzuku kwenye mafuta ya kisukuku na nishati itokanayo na nguvu ya joto.

4. UNEP, WMO, IPCC, UNFCCC, COP… kwa nini vifupisho vyote hivi?

Watoto katika eneo la Merea nchini Chad wakipanda miti kama nija mojawapo ya kukabiliana na kuenea kwa jangwa nchini humo
UNDP Chad/Jean Damascene Hakuzim

Ni kweli kwamba Umoja wa Mataifa umezoa vifupisho. Vifupisho vyote hivi vinawakilisha mikataba na mashirika ya kimataifa ambayo, chini ya uongozi wa Umoja wa Mataifa, yaliundwa ili kusaidia kuendeleza hatua kwa tabianchi ulimwenguni. Hivi ndivyo zinavyoshirikiana.

UNEP ni programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa, ikiwa na mamlaka kuu katika usimamizi wa mazingira duniani na inaweka ajenda ya mazingira ya ulimwengu na hutumika kama mchechemuzi wa masuala ya mazingira duniani. WMO ni shirika la hali ya hewa duniani likiwa na wakala anayehusika na ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya utabiri wa hali  ya hewa, kufuatilia mabadiliko ya tabianchi na kutafiti rasilimali maji.

Mnamo mwaka 1988 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilizitaka UNEP na WMO kuanzisha Jopo la kiserikali la mabadiliko ya tabianchi (IPCC), ambalo linaundwa na mamia ya wataalam, ili kutathmini data, na kutoa ushahidi wa kuaminika wa kisayansi kwa ajili ya mashauriano kuhusu hatua kwa tabianchi.

Vyombo vyote hivyo vitatu vya Umoja wa Mataifa huchapisha ripoti, na katika miaka ya karibuni vimekuwa mara kwa mara vikigonga vichwa vya habari vya kimataifa kadri ambavyo shaka na shuku kuhusu janga la tabianchi nchi linavyozidi kuongezeka.

Na kuhusu mfumo wa mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu tabianchi , UNFCCC, hii ni nyaraka ambayo ilipitishwa katika mkutano wa viongozi kuhusu masuala ya dunia mwaka 1992 mjini Rio de Janeiro, Brazil. Katika mkataba huo, mataifa yalikubaliana ku "kutuliza viwango vya gesi chafu angani" ili kuzuia hatari za shughuli za binadamu kuingilia mfumo wa wa tabianchi.

Hii leo, nchi 197 ni wanachama wa mkataba huo. Kila mwaka tangu mkataba uanze kutumika mnamo 1994, "mkutano wa wanachama wa mkataba au COP, umekuwa ukifanyika ili kujadili jinsi ya kusonga mbele na sasa COP25 inafanyika mjini Madrid, Hispania.

5. Ni nini muhimu wa COP25?

Mahali unakofanyika mkutano wa Umoja wa Mataifa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi COP25 mjini Madrid, Hispania
ifema feria de madrid

Kwa kuwa UNFCCC haukuwa na kanuni za kudhibiti utoaji wa hewa chafuzi kwa nchi moja moja na hakukuwepo na mfumo wa kusimamia utekelezaji wake, taratibu mbalimbali za kuongeza wigo wa mkataba huo zilikuwa zinajadiliwa katika mikutano kadhaa ya COP ikiwemo mkutano wa hivi karibuni wa COP25 huko Paris, UFaransa ambao hatimaye ulipitisha mwaka 2015 makataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi na kuamua kudhibiti kiwango cha ongezeko la joto kisizidi nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi kwa kulinganisha na kiwango cha kabla ya mapinduzi ya viwanda.

COP25 ni mkutano wa mwisho kabla ya kufikia mwaka 2020 ambako mataifa yote yatawasilisha mipango yao mipya ya hatua kwa tabianchi. Kubwa zaidi ni ufadhili kwa ajili ya hatua kwa tabianchi.

Hivi sasa, hatua zinazofanyika hazitoshelezi kufikia kiwango cha kupunguza kwa asilimia 45 utoaji wa hewa chafuzi ifikapo mwaka 2030 na hatimaye kutokuwepo kabisa na  hewa ya  ukaa hewani mwaka 2050 hali itakayofanya kiwango cha joto kisizidi nyuzi joto 1.5.

Kwa kuwa muda unasonga,  ulimwengu hauwezi kumudu kupoteza wakati mwingine, na uamuzi wa thabiti na jasiri na wa makusudi ulikubaliwa ni lazima ufanyike.