Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi zinazoendelea, LDCs, zimeondoka COP25 zikiwa zimevunjika moyo

Vijana wanaharakati walikusanyika mjini Madrid kudai hatua kuchukuliwa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi
UNFCCC
Vijana wanaharakati walikusanyika mjini Madrid kudai hatua kuchukuliwa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi

Nchi zinazoendelea, LDCs, zimeondoka COP25 zikiwa zimevunjika moyo

Tabianchi na mazingira

Mapema leo jumapili mchana huko mjini Madrid, Spain, mkutano wa wanachama wa mkataba wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, UNFCCC, umehitimishwa kwa kupitisha makubaliano yaliyopewa jina ‘Chile Madrid wakati wa kuchukua hatua’, lakini makubaliano hayo yakiwa yameacha masuala mengi bila kutatuliwa na hivyo nchi zinazoendelea hazikuridhishwa.

 

Bwana Sonam P Wangdi, Mwenyekiti wa kundi la nchi zinazoendelea, LDCs, amesema, “mkutano wa 25 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP25 haukuweza kufikia matarajio yetu katika kuongeza hamasa ya kushughulikia wasiwasi wa watu wetu nyumbani na vijana kote ulimwenguni. Sasa wakati wa kujibu ombi la kuwasilishwa kwa michango zilizojiwekea nchi, nchi lazima zifanye maboresho ya malengo na mambo yanayohusiana na michango yao na wanachopanga kufanya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi ifikapo mwaka 2020 ambayo yanatuweka kwenye njia ya kupunguza joto hadi nyuzi joto 1.5 °"

Bwana Wangdi ameongeza kusema, “watu wetu tayari wanateseka kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Jamii zetu kote duniani zinaharibiwa. Uzalishaji wa hewa chafuzi duniani unatakiwa kwa kiasi kikubwa na kwa haraka kupunguzwa ili kudhibiti madhara zaidi, na pia ufadhili wa kifedha unatakiwa kuongezwa ili nchi zetu ziweze kushughulikia vizuri mabadiliko ya tabianchi na madhara yake. Tunapaswa kuona nchi zikitekeleza ahadi zao mwaka ujao. Na tunapaswa kuona uwasilishwaji wa dola bilioni 100 zilizoahidiwa kwa ajili ya mapambano ya mabadiliko yay a tabianchi.”

Kukamilishwa kwa sheria za mifumo ya biashara ya uzalishaji wa hewa chafuzi ulimwenguni chini ya ibara ya 6 ya Mkataba wa Paris, lilikuwa suala muhimu katika mazungumzo yam waka huu ya Madrid lakini pande husika hazikufikia makubaliano kwa mara nyingine tena kuhusu jambo hili ambalo pia lilikwamba katika mkutano wa mwaka jana yaani COP24.

Nchi zinazoendelea, kupitia mwenyekiti wake Bwana Wangdi zimeendelea kulalamika zikitoa mifano, “kuna kutokuunganika vya kutosha kati ya uharaka tunaouona nyumbani na uharaka wa mazungumzo haya. Tumeshuhudia mafuriko Msumbiji na Malawi, ukame nchini Senegal na Gambia, mafuriko Bangladesh na Nepal. Majanga haya yameua watu wengi, kusambaratisha makazi na jamii, kuharibu Mashamba na mazao. Wanasayansi wanasema hali itakuwa mbaya zaidi.Hatua zaidi na misaada vinahitajika zaidi. Lakini hapa baadhi ya nchi zinaonekana zinaonekana kubana wajibu wao chini ya makubaliano ya Paris.”