Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tamko la haki za binadamu lizingatie tamaduni na maadili ya taifa- Balozi Mahiga

Waziri wa Katiba na Mambo ya Sheria wa Tanzania
UN /Aliza Eliazarov
Waziri wa Katiba na Mambo ya Sheria wa Tanzania

Tamko la haki za binadamu lizingatie tamaduni na maadili ya taifa- Balozi Mahiga

Haki za binadamu

Wakati Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Tanzania ikiwa imepata uongozi mpya kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais wa Taifa hilo la Afrika Mashariki, John Magufuli, Waziri wa Katiba na Mambo ya Sheria Dkt. Augustine Mahiga amezungumzia majukumu ya tume hiyo wakati  huu ambapo tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limetimiza miaka 71 tangu  kupitishwa.

Akihojiwa jijini Dar es salam, Tanzania na Stella Vuzo wa kituo cha habari za Umoja wa Mataifa, Balozi Mahiga amesema..

"Kwa muda tulikuwa tunatafuta uongozi lakini hivi karibuni Mheshimiwa Rais ameshateua Tume ya Haki za Binadamu, na hii ina mamlaka na ina uhuru kabisa. Mimi kama waziri wa katiba na sheria , inafanya kazi chini ya usimamizi wangu. Nimefurahi sana Mheshimiwa rais alivyoteua hii kamati baada ya muda mrefu, tulikuwa tumesubiri hio. Ninahakika kwamba hii tume ya haki za binadamu hapa Tanzania ikifanya kazi na wizara yangu, itapata nafasi ya kutetea, kueleza na kutoa tafsiri inayotakiwa, na itakuwa ni sehemu ya kujenga utamaduni wa haki za binadamu katika taifa hili."

Balozi Mahiga akaenda mbali zaidi kuelezea umuhimu wa kuhakikisha  utekelezaji wa tamko hilo linazingatia m aadili na tamaduni za nchi husika.

"Ili haki za binadamu na tamko hili liwe ni sehemu ya maisha ya watu, lazima liingizwe katika mfumo mzima wa utamaduni wa nchi, na mfumo mzima wa uelewa na utetezi wa haki hizo, na kuwa na uhuru wa kutosha kuweza kutetea haki hizi bila kuingiliwa. Lakini kwa sababu linalenga watanzania, ni vizuri kutazama pia utamaduni na lengo na uhuru na sura ya kitanzania. Lakini hio haina maana kwamba tamko hili ni tamko la kila nchi kulingana na historia na utamaduni wake. Ni tamko la kimataifa, lakini uelewa wake na utafsiri na utekelazaji wake utakuwa tofauti kutoka nchi moja na nyingine."

Mwezi Oktoba mwaka huu wa 2019, Rais Magufuli alimteua jaji mstaafu Mathew Pauwa Mhina Mwaimu kuwa mwenyekiti wa Tume hiyo huku Bwana Mohammed Khamis Hamad akiteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti ambapo wawili hao pamoja na makamishna watano waliapishwa tarehe 4 mwezi uliopita wa Novemba.

 

TAGS :CHRAGG, Tanzania, Augustine Mahiga