Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabaraza ya watoto nchini Tanzania yanasongesha haki za watoto

Mwanahabari kijana Rashid Malekela anazungumza na vijana wenzake wa Mwanza Network studio
Mwanza Youth reporter
Mwanahabari kijana Rashid Malekela anazungumza na vijana wenzake wa Mwanza Network studio

Mabaraza ya watoto nchini Tanzania yanasongesha haki za watoto

Haki za binadamu

Ikiwa leo ni siku ya mtoto duniani, maudhui yakiwa sambaza rangi  ya buluu ili kutetea haki za mtoto, mkoani Mwanza nchini Tanzania watoto nao wameshika hatamu kuhakikisha haki  hizo zinapatiwa kipaumbele.

Miongoni mwa watoto hao ni Neema Theonesti mwenye umri wa miaka 14 na Mwenyekiti wa Baraza la Watoto mkoani Mwanza ambaye amesema wanatetea haki za mtoto kwa kuzungumza na viongozi kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa ili kuhakikisha, "wanaweka mabaraza ya watoto kuhakikisha kuwa watoto wanatetewa haki zao na wanafahamu maslahi yao. Lakini pia tunahakikisha viongozi wa serikali wanaweka vipaumbele katika masuala ambayo yanawahusu, mfano katika vikao mbalimbali vya maendeleo ya kata au mtaa, watoto waweze kushirikishwa na kutoa maoni yao ya nini kifanyike ili kuhakikisha maslahi yao yanakwenda mbele."

Neema amesema, "lakini pia  tunashauri viongozi hawa kuanzia ngazi ya kata hadi taifa suala zima la kuhakikisha kuwa watoto wote wanapelekwa shule kwani elimu ndio kila kit una kinafungulia mtoto mwanga na kufahamu mambo yanayomhusu.”

Neema ambaye anasoma kidato cha tatu anasema ana matumaini ya kwamba kupitia ushirikiano huo Tanzania inayozingatia haki za mtoto inawezekana.