Tuamue tuzame na jahazi la mabadiliko ya tabianchi au tuchukue hatua sahihi- Muhammad-Bande

10 Disemba 2019

Ili kulinda kizazi hiki na kijacho dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, basi ni wajibu wa kila mtu kuchukua hatua na kuhakikisha kiwango cha joto duniani hakiongezeki.

Kauli hiyo imesisitizwa leo na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Tijjani Muhammad-Bande kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa mkutano wa 25 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi COP25 unaoendelea mjini Madrid Hispania.

Muhammad-Bande amesema dunia iliafikiana kudhibiti ongezeko la joto kwa nyuzi joto 2 zaidi ya ilivyokuwa kabla ya maendeleo ya viwanda na kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kiwango kinasalia nyuzi joto 1.5. 

Lakini sasa anasema mwenendo wa kimataia wa utoaji hewa chafuzi ukiendelea utaongeza onyo la hatari Zaidi nabinadamu ndio watakaokuwa wahanga wa matukio mabaya ya hali ya hewa akiongeza kuwa, “majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi sasa yako kila kona ya dunia na hayaheshimu mipaka. Tayari yanasababisha gharama kubwa kwa Maisha ya wat una maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na hatua za kimataifa zilizopigwa katika mchakatowa kupunguza umasikini na kuboresha Maisha ya watu sasa uziko katika tishio kubwa.”

Hivyo amehimiza ni muhimu kuhakikisha matokeo yanapatikana sasa, utoaji wa hewa chafuzi kimataifa unahitaji kushughulikiwa sasa na kupunguzwa kwa kiasi kikubwa.

Ameongeza kuwa, "tunahitaji kuchukua hatua za pamoja sasa,tunapaswa kushirikiana na viongozi wa miji na mamlaka za kijamii,makampuni ya biashara, mashirika yasiyo ya kiserikali NGO’s, makundi ya watu wa asili na asasi za kiraia kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika viwango vya kitaifa na kimataifa.”

Rais huyo wa Baraza Kuu amesema ili kubadili kwa kiasi kikubwa matumizi na mfumo wa uzalishaji. “Tunapaswa kuwekeza katika mabadiliko ya kimuundo na mifumo kimataifa ya nishati, usafiri, uzalishaji wa chakula na mifumo ya miji.”

Ameongeza kuwa kuwekeza katika mnepo na njia za kudhibiti mabadiliko ya tabianchi ni muhimu sana hususan kwa nchi na jamii ambazo ziko katika hatari. 

“Ni lazima kuchukua hatua sasa kulinda uhai, Maisha na nyumba ambazo ndio zinahifadhi watu. Hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi zinaweza kusaidia kuinua uchumi kwa dola trilioni ifikapo 2030. Na mabadiliko katika sekta ya nishati pekee yanaweza kuunda jumla ya ajira milioni 11.6”

Amesisitiza kwamba wajibu kwa ajili ya suluhu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni wa kila mmoja”Kupuuza athari za mabadiliko ya tabianchi itakuwa ni kuwaangusha watu wa dunia hii na vizazi vijavyo. Si visiwa vidogo vinavyoendelea na si mataifa makubwa nchi wanachama wanaoweza kusitisha zahma ya mabadiliko ya tabianchi peke yao, tunahitaji kuchukua hatua za pamoja.”

Bwana Muhammad-Bande amesema hatua za kupunguza hatari ya mabadiliko hayo zinauwezekano wa kuwalinda watu wapatao milioni 280 walio katika hatari ya kutawanywa kutokana na kupanda kwa kina cha bahari. 

Ni uamuzi wetu kuzama na jahazi hili au kubadili hatma yetu mara moja na huu ndio wakati wa kuchukua hatua.”

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter