Heko Ethiopia kwa haki za binadamu lakini msibweteke kazi bado ipo:Kaye

9 Disemba 2019

Baada ya robo karne ya ukandamizaji wa haki za binadamu, sasa Ethiopia iko katika safari ya mchakato wa mabadiliko ambayo yanatia moyo lakini pia ni tete na yanastahili msaada wa kimataifa amesema mtaalam wa haki za binadamu baada ya kuzuru nchi hiyo.

Mtaalam maalum wa umoja wa Mataifa kuhusu haki ya uhuru wa maoni na kujieleza David Kaye kupitia taarifa yake ya awali baada ya kukamilisha ziara nchini Ethiopia amesema “chini ya miaka miwili rekodi ya haki za binadamu nchini Ethiopia ilikuwa inatisha, ya ukandamizaji wa asasi za kiraia, kubinya uhuru wa vyombo vya habari na kusweka rumande na jela waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu”.  Kaye amekuwa ni mtaalam maalum wa kwanza wa haki za binadamu kuzuru Ethiopia kwa muktadha huo tangu mwaka 2006.

Ameongeza kuwa ni miezi 18 tu iliyopita waziri mkuu wa taifa hilo Abiy Ahmed ambaye atapokea tuzo ya amani ya Nobel kesho Desemba 10, alianzisha mabadiliko ya kumaliza hali ya dharura nchini humo, kuawaachilia huru waandishi wa Habari na watetezi wa haki za binadamu, kufungua mlango kwa asasi za kiraia na kuanzisha mchakato wa mabadiliko.

“Ethiopia imepiga hatua kubwa kuelekea uhuru wa kujieleza, hata hivyo huu ni mwanzo tu wa mchakato ambao utachukua miaka na miaka ya ahadi za kisheria na kisera, msisitizo wa ushiriki wa umma na ufuatiliaji wa haki za binadamu.”

Hata hivyo wakati wa ziara yake Bwana Kaye amesema amebaini kuenea kwa hofu kuhusu kauli za chuki katika vyombo vya Habari, machapisho na mitandao ya kijamii, na kuwa tishio kwa utulivu wa mchakato wa mabadiliko.

Mwezi Oktoba watu 86 waliripotiwa kuuawa katika machafuko ambayo wengi wanasema ni sehemu ya mazingira ya kauli za chuki na ubaguzi ikiwemo katika mitandao ya kijamii.

Mtaalam huyo huru amesema, “katika muktadha huu wa mabadiliko na machafuko, serikali imeanzisha mswada wa sheria kuhusu kauli za chuki  na taarifa potofu ambazo zinaweza kuathiri mchakato wa muda mrefu wa mabadiliko. Wasiwasi wangu ni kwamba rasimu ya kauali za chuki na taarifa potofu iliyotangazwa, endapo itapitishwa kama ilivyoainishwa , itatishia uhuru wa kujieleza nchini humo na kuchochea badala ya kupunguza mivutano ya kikabila na kisiasa.”

Mtaalam huyo amekaribisha juhudi za kukabiliana na kauli za chuki na kushughulikia taarifa potofu na kutoa mapendekezo kwa serikali ya jinsi gani ya kuichukulia mada hii katika njia ambayo inaenda sanjari na sheria za haki za binadamu.

Mwezi Mei 2020, Ethiopia itafanya uchaguzi mkuu na kwa mantiki hiyo mtaalam huru ametoa wito,”naitaka serikali kutathimini juhudi zake za kuchagiza na kulinda uhuru wa kujieleza, kuchukua hatua imara kukabiliana na mifumo yote ya udhalilishaji, mashambulizi au ghasia dhidi ya waandishi wa Habari, waandamanaji na mtu yeyote anayetekeleza haki yake ya msingi ya kujieleza na pia kuimarisha majadiliano ya kitaifa na kuvumiliana nchi nzima.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud