Tafadhali sitisheni kwanza matumizi ya vifaa vya kuchunguza maisha ya watu-Mtaalamu UN

25 Juni 2019

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa maoni na kujieleza, David Kaye, hii leo ametoa wito wa kuzuiwa haraka kuuzwa, kusafirishwa na kutumiwa kwa teknolojia ya kufuatilia na kuchunguza maisha ya watu hadi pale ambapo mifumo ya udhibiti inayozingatia haki za binadamu itakapokuwepo.

Mtaalamu huyo ametoa mapendekezo hayo katika ripoti yake mpya kwa Baraza la Haki za binadamu kuhusu tasnia ya uchunguzi na namna inavyoingilia haki za binadamu.

Bwana Kaye anasema, “vifaa vya kufuatilia na kuchunguza watu vinaweza kuingilia haki za binadamu, kuanzia haki ya faragha na uhuru wa kujieleza hadi haki ya kujumuika na kukutana, imani za kidini, kutokubaghuliwa, na ushiriki wa kijamii.”

Kaye ametoa mifano ya kuingiliwa kwa mifumo ya kompyuta, simu za mkononi, mitandano, vifaa vya kuchunguza na kufuatilia sura za watu na vifaa vingine vya ubora wa juu ambavyo vimekuwa vikitumiwa na mataifa na watu wengine kuwafuatilia wanahabari, wanasiasa, wachunguzi wa Umoja wa Mataifa na watetezi wa haki za binadamu.

Kutokana na hali ya sasa ya kukosekana kwa udhibiti madhubuti wa matumizi ya vifaa hivyo, ili kudhibiti madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi yake, Bwana Kaye ameongeza kusema, “ni wakati sasa mataifa yaweke mipaka ya matumizi ya teknolojia hizo isipokuwa zile zinazofuata sheria. Ni wakati sasa serikali na makampuni kutambua wajibu wao kwa lengo la kulinda haki za binadamu kwa wote.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud