Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna mpito usio na msukosuko: Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein. Picha: UM/Video capture

Hakuna mpito usio na msukosuko: Zeid

Haki za binadamu

Kamishina Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein amehitimisha ziara yake nchini Ethiopia na kusema licha ya changamoto na misukosuko waliyopitia raia wa nchi hiyo kuna matumaini ya mambo kutengamaa.

Nyakati za mpito katika taifa katu hazikosi misukosuko, lakini hatimaye nuru inaonekana, amesema Zeid Ra’ad Al Hussein mwishoni mwa ziara yake nchini Ethiopia, nchi iliyoshuhudia mvutano wa hali ya juu kati ya serikali na wapinzani. Flora Nducha na ripoti kamili.

(Taarifa ya Flora Nducha)

Kamishna huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema hayo leo mjini Addis Ababa, Ethiopia mwishoni mwa ziara yake ya siku nne nchini humo kufuatia mwaliko wa serikali.

Ametaja misukosuko hiyo kuwa ni pamoja na mvutano kati ya serikali na wapinzani wa kisiasa ambapo baadhi yao bado wamesweka rumande huku wengine wakiachiliwa huru. 

Hata hivyo amesema ameshuhudia mabadiliko makubwa ikiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu ikiwemo Chuo Kikuu cha Addis Ababa  kuzungumza bila woga wakikosoa serikali.

(Sauti ya Zeid Ra’ad Al Hussein)

“Jambo muhimu ni kwamba kunaonekana kuna nia ya dhati ya uongozi wa serikali kuelekea mwelekeo huu na hili ni jambo ambalo tunaunga mkono na kukaribisha kwa uwazi.”

Bwana Zeid amesema baadhi ya wafungwa wa kisiasa, wamemweleza matumaini yao na uongozi mpya wa Ethiopia, lakini bado wanahisi ahadi wanazopatiwa za kuona nuru ni ahadi zisizotekelezwa.

Amesema hivi sasa Waziri Mkuu mpya wa Ethiopia Abiye Ahmed anafanya ziara mikoa mbalimbali ya nchi hiyo kuelezea dira ya serikali yake ya kuleta mabadiliko chanya, na wananchi kwa upande wao..

(Sauti ya Zeid Ra’ad Al Hussein)

“Wana shauku ya kuona yote haya yanafanikiwa na pia wana hofu kuwa pengine kutakuwepo na vikwazo. Hivyo kuna matumaini makubwa lakini pia hofu. Kwa hiyo tunatumia dira ya Waziri Mkuu inatekelezwa vyema.”

Kamishna Zeid amesema Ethiopia imepitia historia ya vuguvugu zito lakini ina busara ya stahmala na vijana wa kuwatumia.