Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lazima turejeshe imani ya suluhu ya mataifa mawili, Palestina na Israel:Guterres

Maonyesho ya picha na ujumbe kutoka kwa watu mashuhuri kuhusu siku ya Kimataifa ya mshikamano na watu wa Palestina kwenye makao makuu ya umoja wa Mataifa New York
UN News/ Shirin Yaseen
Maonyesho ya picha na ujumbe kutoka kwa watu mashuhuri kuhusu siku ya Kimataifa ya mshikamano na watu wa Palestina kwenye makao makuu ya umoja wa Mataifa New York

Lazima turejeshe imani ya suluhu ya mataifa mawili, Palestina na Israel:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameiomba jumuiya ya kimataifa kurejesha imani ya suluhu ya mataifa mawili, Israel na Palestina ili kumaliza miongo ya mzozo wa Mashariki ya Kati.

Katika ujumbe wake maalum wa siku ya kimataifa ya mshikamano na Wapalestina ambayo kila mwaka huadhimishwa Novemba 29, Guterres amesema ameahidi kwamba umoja wa Mataifa “Hautosita katika kutimiza ahadi zake kwa watu wa Palestina na kutoa wito wa uongozi na utashi wa kisiasa katika kutatua moja ya matatatizo na changamoto kubwa inayoikabili jumuiya ya kimataifa hivi sasa.“Hakuna mbadala mwingine unaofaa. Ni fikra hatari sana kudhani kwamba mgogoro unaweza kudhibitiwa au kuhimiliwa.”

Katibu Mkuu pia amekumbusha na kusisitiza kwamba ujenzi wa makazi ya walowezi wa Kiyahudu kwenye eneo linalokaliwa la wapalestina ikiwemo Jerusalem Mashariki hauna uhalali wowote kisheria na ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa.

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Akiunga mkono ujumbe huo Rais wa Baraza Kuu Tijjan Muhammad-Bande amesisitiza kuwa “Katika azma yetu ya amani, lazima tuanze kwa maoni kwamba suluhisho la amani kwa mzozo wa Israeli na Palestina haliwezi kutoka kwa maamuzi ya puande mmoja ambayo ni kinyume na maafikiano ya muda mrefu juu ya suala hilo. Ni lazima pia iwe wazi kwamba lazima kuweko kukomeshwa kwa kila aina ya dhuluma, kutoka kwa chanzo chochote, kwani hasara ya kupoteza maisha ya watu yawe ni ya Wapalestina au Israel ni suala lisilokubalika.”

Bande katika ujumbe wake mbele ya wanachama wa Umoja wa Mataifa hii leo amesisitiza kuwa madai na changamoto zote zinapaswa kushughlikiwa kwa uangalifu, kwa viongozi wote kufanyakazi pamoja ili kuhakikisha wanazuia ukiukwaji wowote wa haki na hatua za kuleta machafuko.

Balozi wa uangalizi wa kudumu wa Palestina Umoja wa Mataifa

Naye mwakilishi uangalizi wa kudumu wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyad Mansour katika mahojiano maalum na UN News kuhusu siku hii ya kimataifa ya mshikamano na Watu wa Palestina amesema maadhimisho ya mwaka huu yamekuja na heshma kubwa ya kuwaenzi watu wote mashuhuri walioshikamana na Wapalestina kwa miongo na miongo na kusisitiza kwamba

Umoja wa Mataifa unapaswa kuendelea kujihusisha na masuala ya Wapalestina hadi pale yote yatakapopatiwa suluhu kutoka pande zote mbili-Riyad Masour”

Ameongeza kusema kuwa baada ya 1947, Umoja wa Mataifa haukuipa Uhuru Palestina , hivyo iliamriwa kuigawanya Palestina katika mataifa mawili na kutatua suala hili ni lazima liwe na suluhu za pande zote mbili.

Amesisitiza kwamba amesisitiza kwamba ulimwengu unaowakilishwa na Umoja wa Mataifa unasimama na usawa wa watu wa Palestina. Hii inamaanisha utumiaji wa haki ambazo zinaweza kutengwa kwa Wapalestina, haki ya kujitawala, uhuru na kurejea kwa wakimbizi kama ilivyohakikishwa na viwango na maazimio ya kimataifa.

Mansour amesema Baraza Kuu liliitangaza tarehe 29 Novemba kuwa siku ya kimataifa ya mshikamano na watu wa Palestina ili kusahihisha ukiukwaji wa haki ulioshinikizwa kwa watu wa Palestina kwa kuwanyika haki yao ya uhuru.

Tarehe 29 Novemba ndiyo tarehe ambayo Palistina iligawanywa mapande mwaka 1947.