Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaongeza muda zaidi wa mikakati ya kudhibiti uharamia kando mwa pwani ya Somalia

Harakati dhidi ya  uharamia zikiendeshwa kwenye ghuba ya Aden na mashariki mwa pwani ya Somalia
U.S. Navy/Ja'lon A. Rhinehart
Harakati dhidi ya uharamia zikiendeshwa kwenye ghuba ya Aden na mashariki mwa pwani ya Somalia

UN yaongeza muda zaidi wa mikakati ya kudhibiti uharamia kando mwa pwani ya Somalia

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo kwa kauli moja limepitisha azimio la kuongeza muda wa mikakati ya kudhibiti vitendo vya uharamia nchini Somalia, hatua ambazo zingalimalizika tarehe 6 mwezi huu wa Desemba.

Mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Vasily Nebenzya amelieleza Baraza hilo lililokutana kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kuwa hatua hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika kudhibiti harakati za uharamia kwenye pwani ya Somalia, hatua ambazo amesema zinatekelezwa na jamii ya kimataifa.

Hata hivyo amesema, “mashambulizi yameendelea kutokea na ndio maana Baraza la Usalama na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wana wajibu wa kupatia umakini suala hilo.”

Balozi Nebenzya amezungumzia umuhimu na uhitaji wa kuendelea kuratibu jitihada za kukabiliana na uharamia kwenye pwani ya Somalia chini ya kikosi kazi maalum chenye jukumu hilo na amesisitiza mfumo huo wa uratibu uendelee.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kudumu wa Somalia kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Mohamed Rabi Yusuf amesema kuwa azma ya dhati ya serikali yake na harakati za jumuiya ya kimataifa kudhibiti uharamai umesaidia kupunguza vitendo hivyo katika miaka ya hivi karibuni.

Hata hivyo amesema kuwa, “uharamia katika pwani ya Somalia lazima uangaziwe katika muktadha wa kisiasa, usalama na changamoto za kiuchumi zinazokabili taifa hilo la pembe ya Afrika”

Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya uharamia na uporaji kwenye maeneo ya bahari kando mwa pwani ya Somalia ambayo imechapishwa tarehe 8 mwezi uliopita wa Novemba imetaja matukio mawili tu ya uharamia kwenye eneo hilo yaliyofanyika tangu tarehe 1 mwezi Oktoba mwaka jana.

TAGS: Somalia, Uharamia, Baraza la  Usalama