Baraza la Usalama la UN lazungumzia kutotakiwa kwa Haysom Somalia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
UN
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Baraza la Usalama la UN lazungumzia kutotakiwa kwa Haysom Somalia

Amani na Usalama

Baada ya Nicholas Haysom, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia kutotakiwa tena nchini humo Baraza la Usalama la umoja huo nalo limepaza sauti.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wametoa taarifa yao na kueleza  masikitiko yao kufuatia kitendo ha serikali ya shirikisho ya Somalia kumtangaza Nicholas Haysom kuwa hatakiwi nchini humo na anapaswa kuondoka.

Wameeleza kutambua taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa  Mataifa siku ya Ijumaa ya tarehe 4 Januari 2019 ikimnukuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Hata hivyo wameelezea shukrani zao kwa Bwana Haysom na kusisitiza uungaji mkono ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi nchini Somalia, UNSOM na mamlaka yake kwa mujibu wa azimio la baraza hilo namba 2408 la mwaka 2018.
 
Halikadhalika wamesisitiza azma ya jamii ya kimataifa ya kuendelea kusaidia mchakato wa amani, utulivu na maendeleo nchini Somalia na kusisitiza kwa minajili hiyo matarajio yao ya kutimiza ushirikiano kamili kati ya Somalia na Umoja wa Mataifa.
 
“Wanachama wamesisitiza kuwa mwaka 2019 utakuwa mwaka muhimu kwa Somalia, na kutoa wito kwa viongozi wa nchi hiyo kushirikiana pamoja kusongesha marekebisho ya kisiasa na kiusalama,” imesema taarifa ya wajumbe hao wa Baraza la Usalama iliyotolewa jumamosi tarehe 5 Januari 2019.

Halikadhalika wajumbe hao wamesisitiza kuendelea kuheshimu uhuru, mamlaka na uhuru wa kisiasa na umoja wa taifa la Somalia.