Wakimbizi kutoka Sudan Kusini walioko DRC waanza kurejea nyumbani mji wa mpakani wa Ezo 

13 Novemba 2019

Wakimbizi kutoka Sudan Kusini waliokimbilia nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wanaendelea kurejea nyumbani kufuatia hali kutengamaa tangu kutiwa saini mkataba wa makubaliano ya amani Septemba 2018.

Katika mpaka wa DRC na Sudan Kusini kuna mji wa Ezo ambako watu karibu saba wanawasili kila wiki ambako wanapimwa na wahudum wa afya kwa ajili ya kuchunguzwa Ebola. Kufikia sasa kaya 1,251 za wakimbizi wanaorejea makwao zimeandikishwa katika mji wa Ezo.

Victoria Emilia ni mama wa watoto saba kutoka Sudan Kusini ambaye alirejea nyumbani Ezo mwezi Machi wakati aliposikia kwamba kuna amani, hata hivyo ukosefu wa shule ulimlazimu kuacha watoto wengine nchini DRC.

“Tulirejea kwa sababu tulisikia kwamba mchakato wa amani unaendelea vizuri, na tulisikia pia kupitia redio kwamba wale waliokuwa wamesaka hifadhi nchi jirani warejee nyumbani. Tuliposikia hivyo, tulifurahi sana kwa sababu nyumbani ni nyumbani na ndiyo sababu tuliamua kurejea.”

Kwa wanaorejea nyumbani hakuna shule lakini takriban watoto sabini wa umri wa kwenda shule waliorejea kutoka DRC wanasomea chini ya miti. Justin mwenye umri wa miaka tisa ni mmoja wao, na ana ndoto kubwa.

“Jina langu ni Justin, niko darasa la nne, ningependa kuwa daktari.”

Walimu wa kujitolea wanaendesha masomo kwa watoto hao bila malipo. Hatahivyo mengi zaidi yanahitaji kufanyika kama anavyosema Christopher Murenga afisa mkuu wa ofisi ya operesheni Yambio

“Shule inahitaji kuimarishwa, kwa sasa ina wanafunzi 68 lakini nadahni idadi inahitaji kuwa juu zaidi. Na hii itakuwa ni muhimu sana kufanya kwa sababu tunafahamu kwamba elimu ni chachu ya maendeleo na ina mchango katika amani, kadri watu wanavyopata maarifa ndivyo kuna uwezekano wa kujihusisha na shughuli za amani, kwa hiyo hili ni moja ya vitu tunavyofuatilia.”

Kwa sasa matumaini ni kwamba amani itasalia nchini Sudan Kusini na kwamba mashirika mbalimbali yatachangia katika kuhakikisha mahitaji muhimu ya jamii kwa watu wanaorejea yanapatikana.

 

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud