Watoto wanatambua haki zao wanachotaka wao ni kwamba zizingatiwe

20 Novemba 2019

Katika kuadhimisha siku hii ya kimataifa ya mtoto, inayokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 30 tangu kupitishwa kwa mkataba wa kimataifa wa mtoto, CRC ambao Tanzania imeridhia na hata kutunga sheria ya mtoto, Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kupitia radio washirika wake imekusanya maoni ya watoto wakiulizwa iwapo wanafahamu haki zao?

Kwanza ni Tarime mkoani Mara, Godlove Mwema anasema, "Haki ya watoto kama mimi hapa, kupelekwa shuleni, kuishi na wazazi wake pamoja."

Naye Rehema Daudi Mnanga anasema, "Kwanza napenda kuzungumzia haki za watoto ya kwanza, kupata elimu, na haki ya pili, kupata mavazi, ya tatu matibabu na ya nne, kupata mahali pa kuishi. Ya mwisho kupewa matibabu."

Filbert Mgoyo wa kijiji cha Magena, anasasema, "katika upande huu wa Magena, haki ambayo watoto hawapewi ni haki ya kushirikishwa katika kuchangia hoja. Mambo mengi yanafanyia hapa katika hiki kijiji huwa yafanyika kwa wazazi kwa wazazi, kwa hivyo watoto huwa hawapewi nafasi sana katika kuchangia mawazo. Na watoto huwa wana nafasi kubwa katika jamii katika kuchangia mawazo."

Na kutoka Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Daniel Elia kutoka Namakonde anasema, "nina umri wa miaka 13. Nasoma darasa la 6, shule ya msingi ya Makonde. Haki za mtoto zina maana nyingi sana kwangu, kwa sababu mimi kama mtoto, nisipopata haki hizo, maisha yangu ya baadaye yatakuwa ya utatanishi. Haki hizo ni kama elimu, na haki ya kuheshimiwa kwa sababu kama hujaheshimiwa, yaani ninaweza nikajidharau nikasema kumbe mimi si kitu kwa watu, yaani mimi siheshimiwi na mimi sina lolote kwa mtu kwa sababu ukiangalia yaani hata mheshimiwa rais naye alikuwa mtoto. Na aliheshimiwa na alilindwa na ndio maana akawa rais."

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter