Zaidi ya watoto 45,000 waliokuwa kizuizini waachiliwa huru: UNICEF

15 Novemba 2021

Uchambuzi mpya uliotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa lakuhudumia watoto- UNICEF umeeleza kuwa zaidi ya watoto 45,000 wameachiliwa huru kutoka kizuizini na kurudishwa kwa familia zao wakiwa salama au kutafutiwa njia mbadala inayofaa kwa malezi ya watoto tangu kuanza kwa janga la COVID-19.

Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Henrietta Fore kutoka jijini New York Marekani ikiwa ni kuelekea kwenye kongamano la dunia la haki za Watoto imeongeza kuwa uchambuzi huo ni Ushahidi tosha kwamba masuluhisho ya haki rafiki kwa Watoto.

"Tumejua kwa muda mrefu kwamba mifumo ya haki haina vifaa vya kushughulikia mahitaji maalum ya Watoto, hali ambayo inazidishwa na janga la COVID-19. Hata hivyo tunapongeza nchi ambazo zilitii wito wetu na kuwaachilia watoto kutoka kizuizini. Kwa kuwalinda watoto kutokana na hali ambazo zingeweza kuwaweka hatarini zaidi kwa ugonjwa mbaya, nchi hizi ziliweza kushinda upinzani wa umma na kuchochea masuluhisho ya haki yanayolingana na umri. Hili limethibitisha jambo ambalo tayari tunajua, suluhu za haki zinazofaa kwa watoto ni zaidi ya iwezekanavyo.” Amesema Fore.

Uchambuzi wapili wa UNICEF umekadiria duniani kote kuna zaidi ya watoto 261,000 wamewekwa kizuizini na kwamba amesihi kuwepo na mageuzi ya haki ya watoto kukomesha uwekaji kizuizini kwa watoto wote.

“Watoto walio kizuizini ikiwa ni pamoja na wale walio chini ya ulinzi kabla na baada ya kesi zao, kwenye vizuizi vya wahamiaji, wale wanaoshikiliwa kutokana na kuhushwa na migogoro ya silaha au usalama wa taifa, au hata wale wanaoishi na wazazi kizuizini mara nyingi huzuiliwa katika maeneo yaliyofungwa na yenye watu wengi.”

Amesema Mkurugenzi huyo Mtendaji wa UNICEF na kuongeza kuwa “Wanakosa fursa ya kupata lishe bora, huduma za afya na huduma za usafi, na wako katika hatari ya kutelekezwa, unyanyasaji wa kimwili na kisaikolojia, na unyanyasaji wa kijinsia. Wengi wananyimwa uwezo wa kupata mawakili na matunzo ya kifamilia, na hawawezi kupinga uhalali wa kuzuiliwa kwao.”

Mvulana anaungana tena na familia yake huko Guatemala baada ya kufukuzwa kutoka Marekani.
© UNICEF/Rodrigo Mussapp
Mvulana anaungana tena na familia yake huko Guatemala baada ya kufukuzwa kutoka Marekani.

Nini Kifanyike

Henrietta Fore amesema wakati watunga sera, watendaji wa sheria, wasomi, mashirika ya kiraia, na watoto na vijana wanapokutana kwenye Kongamano la Dunia wiki hii, ni lazima washirikiane kukomesha uwekaji kizuizini wa Watoto.

Lakini pia ametoa mapendekezo ya kufanyiwa kazi na serikali pamoja na mashirika wakati wanafikiria upya kuhusu haki kwa Watoto, na kukomesha ufungwa kwa watoto wote ambapo miongoni mwazo ni pamoja na:-
1.    Kukomesha kuzuiliwa kwa watoto, ikijumuisha kupitia marekebisho ya kisheria ili kuongeza umri wa kuwajibika kwa uhalifu.
2.    Kupanua usaidizi wa kisheria bila malipo, uwakilishi na huduma kwa watoto wote.
3.    Kuanzisha mahakama maalumu zinazofaa kwa watoto, na mahakama za mtandaoni na zinazohamishika.
4.    Kuhakikisha haki kwa watoto walionusurika kwenye unyanyasaji wa kijinsia, unyanyasaji au unyonyaji, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika michakato ya haki inayozingatia mtoto na kijinsia.
5.    Wawekeze katika ufahamu wa haki za kisheria kwa watoto katika mifumo ya haki na ustawi, hasa kwa watoto waliotengwa zaidi.

"Mtoto yeyote anayezuiliwa ni ushahidi wa mifumo iliyofeli, lakini kutofaulu huko kunaongezwa zaidi. Mifumo ya haki iliyokusudiwa kuwalinda na kusaidia watoto mara nyingi huongeza mateso yao,” alisema Fore.

Kusoma zaidi na kupakuwa ripoti hiyo bofya hapa

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter