Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 30 ya CRC tuhakikishe kila mtoto anapata kila haki- Guterres

Katika kuadhimisha siku ya mtoto duniani , watoto katika kijiji cha Sakassou Côte d'Ivoirewamepanga rangi ya blu shule yao mpya. shule hiyo imejengwa kwa matofali ya plastiki
© UNICEF/Frank Dejong
Katika kuadhimisha siku ya mtoto duniani , watoto katika kijiji cha Sakassou Côte d'Ivoirewamepanga rangi ya blu shule yao mpya. shule hiyo imejengwa kwa matofali ya plastiki

Miaka 30 ya CRC tuhakikishe kila mtoto anapata kila haki- Guterres

Haki za binadamu

Leo ni siku ya mtoto duniani ambapo Umoja wa Mataifa umetaka hatua zichukuliwe kila pahali ulimwenguni ili kila mtoto popote pale alipo aweze kupata haki zake za msingi za kuishi, kuendelezwa, kushiriki na kulindwa.

Ikienda sambamba na maadhimisho ya miaka 30 tangu kupitishwa kwa mkataba wa haki za mtoto duniani, siku hii imetoa fursa kwa Umoja huo kupitia Katibu wake Mkuu Antonio Guterres kupatia msisitizo mkataba huo, CRC ambao ulieleza bayana haki za msingi za mtoto wa kike na wa kiume.

Guterres amesema nchi zote zilitambua hali ya hatari ya kipekee inayokabili watoto na kuahidi kuwapatia chakula, huduma ya afya, elimu na ulinzi na kwamba tangu wakati huo, kumekuwepo na maendeleo .

Mathalani amesema idadi ya vifo vya watoto imepungua kwa zaidi ya nusu na udumavu wa watoto ulimwenguni umepungua ingawa bado mamilioni ya watoto bado wanakabiliwa na vita, umaskini, ubaguzi na magonjwa. 

Hata hivyo amesema,“ ulimwenguni kote, watoto wanatuonyesha uthabiti na uongozi wao wakichechemua ulimwengu endelevu zaidi kwa wote. Tunapoadhimisha miaka 30 ya mkataba huu muhimu, nasihi nchi zote zitime ahadi zao.Tusongeshe maendeleo tuliyofikia na tuahidi kujali watoto kwanza. Kila haki kwa kila mtoto.”

Nchini Jamhuri ya Congo, katika kuadhimisha miaka 30 ya CRC watoto walijitokeza kuchora haki zao.
© UNICEF/UN0346146/Diefaga
Nchini Jamhuri ya Congo, katika kuadhimisha miaka 30 ya CRC watoto walijitokeza kuchora haki zao.

Je wajua siku hii kwa mara ya kwanza ilianzishwa lini?

Siku ya mtoto duniani ilianzishwa mwaka 1954 na huadhimishwa tarehe 20 mwezi Novemba ya kila mwaka ili kusongesha utangamano na ustawi wa kimataifa miongoni mwa watoto wote duniani.

Tarehe hii ni muhimu kwa kuwa ndio ambayo mwaka 1959 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio la Haki za Mtoto na pia ni tarehe ambayo mwaka 1989 Baraza Kuu la Umoja wa  Mataifa lilipitisha mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC.

Tangu mwaka 1990, siku ya kimataifa ya mtoto imekuwa ikiadhimishwa kutambua tarehe hiyo 20 ya mwezi novemba ambapo Baraza Kuu lilipitisha azimio kuhusu haki za mtoto na pia Mkataba wa kimataifa kuhusu haki za mtoto.

Ni vyema kutambua kuwa akina mama, baba, walimu, madaktari, viongozi wa serikali, wanaharakati, viongozi wa dini, viongozi wa kampuni, wanahabari nguli pamoja na vijana na watoto wenyewe wanaweza kuwa na dhima muhimu katika kuifanya siku hii ya kimataifa ya mtoto iwe muhimu zaidi kwenye jamii na nchi zao.

Siku hii pia ni hamasa pia katika kuchechemua na kufurahia haki za mtoto, na kuziweka kivitendo na hivyo kufanya dunia iwe bora zaidi kwa watoto.