Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kabla ya msaada wa IOM tulilazimika kwenda umbali wa kilometa 450 kusaka huduma za afya- Mkazi Yemen

Kadri mzozo unavyoshika kasi Yemen, raia ndio waumiao zaidi na maisha ya watoto wachanga yako hatarini kama ilivyo pichani kwenye hospitali ya Alsadaqah mjini Aden. IOM imeingilia kati kusaidia.
©UNICEF/Saleh Baholis
Kadri mzozo unavyoshika kasi Yemen, raia ndio waumiao zaidi na maisha ya watoto wachanga yako hatarini kama ilivyo pichani kwenye hospitali ya Alsadaqah mjini Aden. IOM imeingilia kati kusaidia.

Kabla ya msaada wa IOM tulilazimika kwenda umbali wa kilometa 450 kusaka huduma za afya- Mkazi Yemen

Afya

Wakati wananchi wa Yemen wakiendelea kuhaha kusaka huduma za afya kufuatia mzozo uliodumu kwa zaidi ya miaka minne sasa, shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, limechukua hatua kuhakikisha huduma za dharura za afya zinaendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, msemaji wa IOM Joel Millman amesema huduma hizo ni pamoja na zile za kuwezesha raia kuonana na daktari na kwamba, “IOM imetoa huduma kwa watu milioni 1 na elfu 95 ambao ni wakimbizi wa ndani, wahamiaji na waliokumbwa na mzozo kuonana na daktari kwa kipindi cha mwaka huu kinachoishia wiki iliyopita.”

IOM inasema kuwa hivi sasa nchini Yemen ni nusu tu ya vituo vya afya ndio vinafanya kazi, na hivyo kusababisha wagonjwa kusafiri umbali mrefu kusaka huduma hizo muhimu na wengine wakizikosa kabisa.

“Kabla ya mzozo kuanza mwaka 2015, tayari huduma za afya zilikuwa zimeshazorota na hii leo ukosefu wa fedha, madaktari, dawa na vifaa vya matibabu umesababisha hali kuwa mbaya zaidi ilhali idadi kubwa ya watu wanaosaka huduma kwenye vituo imesababisha vituo hivyo kuzidiwa uwezo,” amesema Bwana Milman.

Huko Sana’a Yemen, mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Maryam, amesema kuwa, “maisha yetu ni magumu ukiangalia kipato, elimu, huduma za afya, maji na usafiri.”

Maryam ambaye anaishi huko Birali jimboni Lahj anashukuru IOM kwa huduma ambazo wamewaletea kwani hivi sasa huduma za afya zimerejea akifafanua kuwa, “Tulipokuwa hatuna vituo vya afya, tulilazimika kusafiri hadi Hadramout takribani kilometa 120 au Aden takribani 450 kutoka hapa, mwanamke mwenye  uchungu hakuweza kutembea umbali huo.”

Kile ambacho IOM  imefanya ni kuimarisha vituo vya afya vya umma ili viweze kumudu janga linaloendelea. “tunasaidia vituo vya afya kwa kuhakikisha kuwa vinaweza kutoa huduma za msingi kwa jamii zilizo karibu kwa kujengea uwezo wahudumu, kuvipatia dawa na vifaa vya matibabu.”

Halikadhalika IOM inasaidia kurejesha upya vituo 86 nchini Yemen ili viweze kutoa huduma bora, na bure kwa kuhakikisha vinatoa huduma ya kuona daktarin kwa watu 120,000 kila mwezi.