Skip to main content

WHO yaimarisha huduma ya afya huku mgogoro ukishika kasi Hodeidah

Familia nchini Yemen wapata lishe muhimu mara moja tu kwa siku. Picha: WFP

WHO yaimarisha huduma ya afya huku mgogoro ukishika kasi Hodeidah

Amani na Usalama

Hali ya usalama na kibinadamu  ikiendelea kuzorota nchini Yemen,  hususan  mji wa bandari wa Hodeidah, WHO imechukua hatua ili kuhakikisha huduma za afya zinaimarika.

Wakati mgogoro katika jimbo la Hodeidah nchini Yemen unaongezeka, idadi ya watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu ikiwemo  huduma za afya  nayo inaendelea kuongezeka.

Ni kwa mantiki hiyo shirika la afya ulimwenguni, WHO kupitia mwakilishi wake nchini Yemen limesema, linasaidia hospitali nne za umma katika mji wa Hodeidah ili  kuhakikisha kuwa zina uwezo wa kupokea na kutibu majeruhi.

“Sasa tunaendelea kutoa msaada kwa kutoa magari ya kupeleka wagonjwa  hospitali na kupelekwa kwa haraka kwa watoa huduma kufikia watu ambao hawawezi kusafiri kufika vituo vya matibabu, na tunafanya kazi ili kuanzisha vituo vya kutibu majeraha katika maeneo muhimu, "amesema Dkt. Nevio Zagaria, mwakilishi wa WHO,Yemen.

Kabla ya kuzuka kwa machafuko, huduma ya afya katika jimbo hilo ilikuwa ni miongoni mwa mbaya sana. Kwa sasa, wilaya kadhaa huko Hodeidah zinaripoti idadi kubwa zaidi ya matukio ya kipindupindu, pamoja na viwango vya juu sana vya utapiamlo uliokithiri.

Image
Mtoto anahudumiwa katika hospitali ya Sab'een huko Sana'a nchini Yemen. Ni mmoja wa watoto waathirika wa kipindupindu. Picha: © UNICEF/UN065873/Alzekri

WHO pia imeanzisha vituo 7 vya kutoa lishe maalum kwa watoto wanaougua  utapiamlo uliokithiri, vifaa kwa ajili ya matibabu ya watu 200,000, huku dawa kadhaa ikiwemo za kutibu kipindupindu, zimetengwa tayari kusambazwa pindi zitakapohitajika.

WHO imesema wakati hatima ya nchi hiyo inajadiliwa katika ngazi za kimataifa, ukweli ni kwamba mashinani hali ni mbaya mno na kadri mgogoro unaongezeka, ndivyo uwasilishaji wa huduma za afya unahitajika. 

Kwa mujibu wa WHO huduma za msingi za afya zinatakiwa kuhakikishiwa kwa kundi la watu walio hatarini zaidi, kama vile wanawake na watoto, na wagonjwa wanaosumbuliwa kwa muda mrefu magonjwa kama vile kisukari na shinikizo la damu.