Apu ya Tap2Eat yasaidia kufanikisha SDGs Kenya

11 Novemba 2019

Hii leo shule  ya msingi ya Ruiru iliyoko jijini Nairobi nchini Kenya imekuwa na mgeni ambaye ameshiriki katika tukio la kuwagawia wanafunzi mlo wa mchana.

Mgeni huyo si mwingine  bali ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed ambaye lengo la ziara hiyo pamoja na kuwagawia wanafunzi chakula, ilikuwa pia kushuhudia jinsi taasisi ya Food For Education au mlo kwa ajili ya elimu ilivyobuni apu ya Tap2Eat na kuleta  mapinduzi makumbwa katika kuwezesha wanafunzi kupata mlo wakiwa shuleni.

“Nafurahi sana kuwepo hapa hii leo katika shule ya msingi ya Ruiru kusherehekea na kujionea ubunifu, ubia na  ujasiriamali. Nipo hapa kwa sababu ninyi nyote mmeshirikiana kusaka suluhu kwa ajili ya watu na sayari,”  amesema Bi. Mohammed.

Tap2Eat ni apu ambayo inatumia teknolojia ya juu kuwezesha wanafunzi wa shule ya msingi kupata lishe bora. Kupitia apu hiyo, wazazi wanalipa shilingi 15 za Kenya sawa na dola senti 15 kwa mlo ambapo Naibu Katibu Mkuu amesema, Wawira Njiru, ambaye ni muasisi wa shirika hilo la Food For Education pamoja na apu hiyo ya Tap2Eat na wadau wao ni mfano wa  jinsi  ya kupatia watu kipaumbele “na hapa ni vijana ikiwemo watoto wa shule hii.”

UNEP/Jane Smith
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed akimtazama mwanafunzi wa shule ya msingi Ruiru wakati akila mlo unaopatikana kupitia apu ya Tap2Eat

Tunafahamu kuwa pindi watoto wana  njaa, hawawezi kusoma. Kudumaa na kudhoofu kwa mwili kunaathiri zaidi ya watoto milioni 200 kote duniani na hivyo kufanya vigumu sana kwa mtoto kuishi na kumakinika shuleni. Kubadili mwelekeo huu si jambo rahisi, tunahitaji hatua za kipekee zaidi,” amesema Bi. Mohammed na ndipo akamtaja Bi. Wawira.

Amesema kuwa, “tunahitaji watetemeshaji kama Wawira Njiru ambao wanatutoa kwenye fikra za kawaida. Tap2Eat—Food For Education imeleta ujuzi wa kipekee kutoka sekta mbalimbali kwa muktadha wa malengo ya maendeleo endelevu na mpango wa utekelezaji utokanao na mkutano wa kimataifa wa watu na maendeleo, ICPD.”

Bi. Mohammed amesema mpango huo, wadau hao kwa pamoja wanatekeleza malengo ya  maendeleo endelevu, namba 1, kuhusu kutokomeza umaskini, namba 2 la kutokomeza njaa, namba 3 la afya bora, namba 4 la elimu bora.

Watoto wanaonufaika na mpango huo wanakuwa wamevalishwa bangili ya rangi ya chungwa ambapo kabla ya kula simu ya mkononi inaelekezwa kwenye bangili hiyo inasoma data na mtoto anapatiwa chakula.

“Hivi sasa watoto 10,000 kila siku nchini Kenya wanapatiwa chakula, na kwa kuptia bangili hiyo siyo tu wao wananufaika bali pia wakulima wa eneo jirani ambako mazao yao ndio yanapikwa kuwa chakula na pia wapishi wa jirani ndio wanapikia watoto,” amesema Bi. Mohammed,

Amekumbusha kuwa anayepata mlo leo atamkwamua mtu mwingine kutoka kwenye njaa kesho yake na pia kusaidia kubadilisha dunia.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, kudumaa miongoni mwa watoto hugharimu bara la Afrika dola bilioni 25 kila mwaka.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud