Mkutano wa nne wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa ukiendelea huko Nairobi, Kenya, Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo Amina J. Mohammed ametaka mwaka huu wa 2019 uwe mwaka wa kuibuka na suluhu zenye mabadiliko dhidi ya uharibifu wa mazingira.
Akihutubia washiriki kwenye mkutano huo mjini Nairobi, Kenya, Bi. Mohammed amesema hata hizo ni muhimu na zitadhihirishia dunia kuwa siyo tu ni muhimu bali pia inawezekana kubadilisha mfumo wa uchumi duniani ambao unalipa wale wanaojali mazingira na unachukia taka na uchafuzi.
Ametaja maeneo matatu ambayo yanahitaji suluhu bunifu ili kukabiliana na changamoto za mazingira ambapo eneo la kwanza ni ulaji na uzalishaji endelevu kwenye mnyonyoro wa usambazaji wa bidhaa.
Ametolea mfano mwaka 2017 akisema rasilimali zilizochimbwa ardhini kwa ajili ya matumizi zilifikia tani za ujazo bilioni 90, lakini ni chini ya asilimia 10 tu ya rasilimali hizo zilirejelezwa na kutumika tena kwenye uchumi.
Bi. Mohammed amesema ni lazima kubadili tabia ya chukua, tengeneza na tumia mara moja na tupa.
Amepongeza hatua ya hoteli za Hilton ya kupunguza m atumizi ya maji na taka kwa asilimia 50.
Eneo la pili ni kulinda bayonuai akisema ni vyema kutumia vyema ardhi kuchochea uchumi ili kuhakikisha inasalia kwa vizazi vijayo.
Mabadiliko ya tabianchi nchi ndio eneo la tatu akisema hatua za haraka zinahitajika ili kulinda sayari dunia kwa kupunguza hewa chafuzi.
Ametoa mfano wa Nigeria akisema mradi wa majaribio wa vituo vidogo vya kuzalisha umeme kwenye majimbo matano nchini humo unawezesha vijiji kuunganishwa kwenye umeme wa uhakika na usiotoa hewa ya ukaa.
Huko Singapore nako serikali imeongeza kasi ya kupanda miti ili kuepusha matumizi ya viyoyozi ambavo husababisha hewa chafuzi.
Ametaja pia suala la ubia akisema ndio hatua mujarabu kusongesha kazi ya pamoja akisema, “serikali lazima ziweke fursa za kuweza kuchukua hatua za utekelezaji.”
Rais Uhuru Kenyatta
Akihutubia mkutano huo uliohudhuriwa pia na marais akiwemo Manuel Macron wa UFaransa na Maithripala Sirisena wa Sri Lanka, mwenyeji Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema maudhui ya mkutano huo, suluhu bunifu za kukabili changamoto za mazingira, yamekuja wakati muafaka.
“Mabadiliko ya tabianchi yanamweka kila mtu katika hatari kubwa, ni lazima tujumuishe hatua za dhati za kukabiliana nayo hivi sasa sambamba na kuzingatia maendeleo endelevu katika jitihada zetu za kufanikisha mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi na ajenda 2030.”
Rais Kenyatta ametumia hotuba yake pia kushukuru Baraza hilo la Mazingira la kutambua kazi inayofanywa na vikundi viwili vya kiasili nchini Kenya vya kuhifadhi na kutunza mazingira kwa kupigia chepuo matumizi endelevu ya rasilimali.
Ametaja vikundi hivyo ambavyo vimekuwa vikionyesha kazi zake kandoni mwa mkutano huo, kuwa ni “kikundi cha Mikoko Pamoja kutoka ukanda wa pwani, kinahifadhi, kinasimamia na kinaimarisha misitu ya mikoko ilhali kikundi cha ubunifu cha pwani kinahifadhi mimea ya chini ya baharí.”