Tuache uraibu wa makaa ya mawe- Guterres

2 Novemba 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka mataifa yaache uraibu wa makaa ya mawe kwa sababu ndio tishio kuu katika tabianchi.

Guterres amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari mjini Bangkok, Thailand kabla ya kuanza kwa mkutano wa mwaka wa viongozi wa jumuiya ya nchi za kusini-mashariki mwa Asia, ASEAN.

“Kuna uraibu wa makaa ya mawe ambao tunapaswa kuachana nao kwa sababu umesalia kuwa tishio kubwa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na moja ya ujumbe utakaokuwa dhahiri kwenye mkutano huu ni kwamba nchi zilizopo eneo hili ziko katika moja ya maeneo hatari zaidi kwa mabadiliko ya tabianchi zinapaswa kuonesha mfano,” amesema Katibu Mkuu.

Ameongeza kuwa nchi hizo zionyeshe mfano kwa kutoza hewa ya ukaa, ziache kuweka ruzuku kwenye mafuta ya kisukuku na pia ziache kujenga mitambo ya kuzalisha umeme inayotumia makaa yam awe.

Bwana Guterres amesema kwa kufanya hivyo nchi hizo zitakuwa zimekabili mabadiliko ya tabianchi na kulinda miji mizuri kama vile Bangkok na mingineyo ambayo inataiwa kutunza mandhari yake kwa binadamu.

Bangkok imekuwa mfano ambapo kuna bustani maalum yenye miti na mazingira ya kijani, mradi ambao Bwana Guterres ametembelea na kusema ni mfano wa kuigwa.

Uendelevu kuwa kitovu cha mjadala ASEAN

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa katika mkutano huo wa ASEAN, suala la uendelevu ndilo litakuwa msingi wa majadiliano akisema kuwa, “tishio kubwa la uendelevu duniani hivi sasa ni mabadiliko ya tabianchi. Siku chache tu zilizopita kituo kimoja cha utafiti kimechapisha ripoti inayosema kuwa kiwango cha maji ya bahari kinaongeza kwa kasi kubwa kuliko ilivyotabiriwa kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi. Ripoti hii inasema kuwa tusipoweza kubadili mwelekeo huu ifikapo mwaka 2050 maji ya bahari yatafurika na kuathiri watu milioni 300 duniani kote.”

Amesema maeneo yaliyo hatarini zaidi ni yale ya kusini-mashariki mwa Asia, Japan, China, Bangladesh na India na kwamba, “kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 10 ya wananchi wa Thailand watakuwa wanaishi kwenye maeneo yaliyofurika maji ya bahari.”

Bwana Guterres amesema watu wanaweza kujadili usahihi wa takwimu  hizo lakini ni dhahiri  mwenendo huo ndio uliopo sasa na jibu pekee ni utashi wa kisiasa kupunguza hewa chafuzi.

Waandishi wa habari walimuuliza Katibu Mkuu juu ya mvutano hasa katika matumizi ya maji ya mito hususan mto Mekong ambao hivi sasa kiwango cha maji kimepungua na mataifa kama China na Laos yanapanua ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha nishati ya umeme.

Bwana Guterres amesema swali hilo limemkumbusha wakati akiwa Waziri Mkuu wa Ureno ambapo taifa hilo lilitia saini makubaliano na Hispania ya matumizi bora ya maji ya mito inayotumiwa kwa pamoja na nchi hizo na hivyo amesema, “wito wangu kwa mataifa yaliyopo kwenye eneo hilo la mto Mekong wawe na mpango mmoja wa matumizi ya rasilimali ya maji, mpango ambao utanufaisha pande zote .Nashauri kwa dhati mazungumzo na ushirikiano.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud