Misri acheni msako dhidi ya watetezi wa haki za binadamu- Wataalamu

28 Oktoba 2019

Wataalamu 7 wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameitaka Misri ilinde uhuru wa wananchi kujieleza, kukusanyika kwa amani na kujiunga kwenye vikundi wakati  huu ambapo taifa hilo limeshuhudia mlolongo wa matukio ya kukamatwa kwa waandamanaji, wanahabari na watetezi wa  haki za binadamu nchini humo.

Kauli hiyo ya wataalamu hao huru wa haki za binadamu imo kwenye taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa na inatokana na hatua ya vikosi vya usalama vya  Misri kuchukua hatua dhidi ya waandamanaji tarehe 20 na 21 mwezi uliopita wa Septemba ambapo waandamanaji  hao walikuwa wanataka Rais Abdel Fattah al-Sisi ajiuzulu sambamba na kutaka ukomo wa ufisadi serikali na hatua za kupunguza matumizi.

Wataalamu hao ni Michel Forst,  David Kaye,  Leigh Toomey,  Agnes Callamard, Fionnuala Ní Aoláin, Clement Nyaletsossi Voule na  Nils Melzer.

“Tunaelezea hofu yetu juu ya nguvu kupitia kiasi iliyotumiwa na vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji,” wamesema wataalamu  hao wakiongeza kuwa, askari hao walitumia silaha za moto, risasi bandia na mabomu ya kutoa machoni na kwamba takribani tangu kuanza kwa maandamano hayo watu 3,000 wamekamatwa.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, walioswekwa korokoroni ni pamoja na waandishi wa habari, waandamanaji, wanazuoni, na watetezi mashuhuri wa haki za binadamu, “na wengi wao wanakabiliwa na mashtaka na yadaiwa wamenyimwa haki ya kuwakilishwa kisheria.”

Wataaamu hao wamekumbusha kuwa jukumu la msing ila mamlaka za usalama ni kulinda waandamanaji ili maandamano yafanyike kwa amani na kwamba, “matumizi ya nguvu hayaruhusiwa ila pale tu ambapo ni  lazima kufanya hivyo na si kwa kiasi kikubwa kuzidi kiwango kinachotakiwa. Matumizi ya risasi za moto yanapaswa kuwa hatua ya mwisho kabisa.”

Wamekumbusha kuwa matumizi ya sheria dhidi ya ugaidi katika kulenga watu waliochoshwa na mwenendo wa serikali au wanaosaka kusongesha haki za binadamu katu si sahihi kwa mujib uwa sheria za haki za binadamu.

Hata hivyo wamesema wasiwasi wao mkubwa zaidi ni ripoti ya kupigwa na kauli za fedheha dhidi ya watetezi mashuhuri watatu wa haki za binadamu ambapo ni Alaa Abdel Fattah, Mohamed El-Baqer na Esraa Abdel Fattah ambao wanashikiliwa na tayari wamefunguliwa mashtaka.

Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa serikali ya Misri kuchungua kwa kina madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na ichukue hatua dhidi ya waliotekeleza vitendo hivyo, “na pia tunasihi serikali isake njia bora zaidi za kushirikisha jamii katika kutatua machungu yanayowakabili.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud