Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misingi ya kupatia raia nyumba Misiri isiwe ya kibaguzi- Mtaalam wa UN

 Bendera ya Misri
UN Photo/Loey Felipe
Bendera ya Misri

Misingi ya kupatia raia nyumba Misiri isiwe ya kibaguzi- Mtaalam wa UN

Haki za binadamu

Misri imepiga hatua mbele kuweza kutanzua suala nyeti la tatizo la nyumba, ingawa hivyo bado kuna safari ndefu ili kila raia aweze kupata haki yake ya msingi ya kuwa na nyumba.

Ni kauli ya mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya nyumba, Leilani Farha, aliyotoa leo huko Cairo, Misri mwishoni mwa ziara yake nchini humo.

Taarifa imemnukuu akisema kuwa takriban watu milioni 38 nchini Misri wanaishi katika makazi yasiyo na mpangilio wowote huku mipango ya kuboresha hali ya makazi yao ikiwa ni midogo mno.

Bi. Farha amesema kuwa, “Misri, taifa lenye wahandisi na wasanifu majengo waliobobea na umahiri wa kufyatua matofali lakini bado wanahitaji kujua umuhimu, thamani na machango wa mwanadamu ili haki zake za  kupata nyumba kuweza kutambuliwa.”

Ameongeza kuwa, “ yaonekana kama Misri  inachukulia maanani azma zake chini ya lengo 11 la maendeleo endelevu. Rais mwenyewe aliazimia kujenga makazi milioni moja na kuboresha makazi ya walala hoi. Serikali imeunda fuko la nyumba za jamii na hili linaweza kuwa kama mfano kwa mataifa mengine.”

Hata hivyo amesema bado njia nyingine bunifu za ukarabati wa  ujenzi wa nyumba za jamii hazijajaribiwa ipasavyo.

Amesema kuwa ili kuweza kukabiliana vilivyo na makazi ya mabanda , serikali  imeanza mkakati wa  kujenga miji mipya 42.

Ingawa hivyo amesema changamoto ni kwamba wananchi wamehamishiwa maeneo mengine ya mbali na maeneo yao ya kazi na pia  mitandao yao  ya kijamii huku wananchi hao wakiwa hawashirikishwi vya kutosha katika mipango hiyo ya makazi.

Amegusia pia jambo moja aliloona ni kasoro katika mgao wa makazi nchini Misri kuwa ni ubaguzi kwa kundi la watu waliobadili jinsia au wapenzi wa jinsia moja, LGBTI akisema kuwa “hawathaminiwi kuhusu masuala ya nyumba. nimesikia taarifa za kusikitisha kuhusu kundi hili kama vile kushambuliwa na kubaguliwa jambo ambalo linasababisha watu hawa kukosa makazi.”

Amesema kuwa  ni sharti serikali ya Misri itambue haki za ma LGBT na kuwapatia ulinzi sawa pamoja  na haki  sawa ya kupata nyumba kama watu wengine.