Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Posta na intaneti kuendelea kuwa sambamba- Ripoti

Msifunge masanduku ya barua kwani yataendelea kuhitajika.
UPU
Msifunge masanduku ya barua kwani yataendelea kuhitajika.

Posta na intaneti kuendelea kuwa sambamba- Ripoti

Ukuaji wa Kiuchumi

Huku kasi ya teknolojia ya mawasiliano ikizidi kuongezeka, baadhi ya watu wamekuwa wakidhani kuwa sasa kifo cha huduma za posta kimewadia. Hata hivyo ripoti ya leo inaonyesha kuwa posta na intaneti vitaendelea kuwa sambamba na kuhitajiana zaidi na zaidi.

Utafiti mpya uliotolewa leo unaonyesha kuwa huduma za posta bado zinasalia kuwa injini kuu ya kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGS na kuchochea uchumi wa nchi duniani.

Ikiangalia vigezo vikuu vinne ambavyo ni kutegemewa, kufikika, umuhimu na mnepo, ripoti imemulika nchi 173 na kuona ni jinsi gani kule ambayo huduma za posta zimepatiwa kipaumbele, maendeleo nayo yameshamiri.

Uswisi imeshika nafasi ya kwanza kwa kuwa na mtandao wa posta ambao siyo tu unatumika katika eneo kubwa bali pia unatoa huduma tofauti tofauti. Uholanzi ni ya pili ikijinasibu na kasi kubwa ya kufikisha barua na vifurushi na ushirikiano wake mkubwa na wadau wa kimataifa.

Japani ni ya tatu na imeshika nafasi hiyo kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma hizo nchini humo sambamba na ubora wake. Kwa bara la Afrika Nigeria ni ya kwanza kwa huduma bora za posta.

Akizungumzia ripoti hiyo, Bishar A. Hussein ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa shirika la posta duniani amesema  ripoti hiyo inaonyesha ni jinsi gani mtandao bora wa posta unaweza kuchagiza maendeleo.

Mathalani huduma za kibenki zinatekelezwa na mtandao wa posta na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika maendeleo ya mifumo ya kifedha duniani.

Ripoti imebainisha uhusiano mkubwa kati ya kasi ya intaneti na huduma za posta ikisema kuwa watu wengi hivi sasa wananunua bidhaa kupitia mtandao na vifurushi vyao kuwasilishwa makwao kwa njia ya posta.

Kwa mantiki hiyo ripoti inasema mwelekeo hivi sasa ni kuimarisha mtandao wa intaneti sambamba na huduma za posta.