Mabilioni ya barua na vifurushi bado yanategemea posta kila mwaka:UPU
Posta bado ina mchango mkubwa kote duniani kwa maisha ya watu na maendeleo endelevu ambapo kila mwaka husafirisha barua bilioni 368.4 na vifurushi bilioni 6.4
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, katikakuadhimisha siku ya Posta duniani ambayo kila mwaka huwa Oktoba 9.
Katika ujumbe wake kwa siku hii, Bw Guterres, amesema sekta ya Posta ambayo ina ofisi zaidi ya 600,000 duniani kote, ni moja ya vituo vyenye mtandao mkubwa duniani ambao ni muhimu kwa maisha ya jamii.
Amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu, ni ishara ya thamani ya sekta hiyo sio tukatika kusafirisha barua tu lakini pia mizigo.
Mfumo wa posta uliothabiti, amesema Katibu Mkuu hutoa msaada wakati wa majanga, pia hutoa huduma za kifedha kwa mamilioni ya watu, na hutoa habari muhimu kwa watu hususan wakati wa migogoro.
Ameongeza kuwa mtandao huu, ni sauti ya ushirika na pia chombo cha msukumo wa ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu ikiwa ni pamoja na kusaidia kukuza usomaji na elimu kwa watoto.
Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa ofisi ya kimataifa ya Muungano wa Posta duniani UPU- Bishar A. Hussein, anasema, kila siku duniani kote huduma za posta zinachangia kitu kipya katika maisha ya watu na jamii. Hii ni kutokana na utoaji wake wa huduma muafaka, za bei nafuu na zenye kuaminika duniani kote.
Ameongeza kuwa posta ni daraja la kuiunganisha jamii kwa kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma kupitia mitandao yake hata na wale waishio katika sehemu za mashambani, katika visiwa na pia katika maeneo yenye majanga.
Na kwa watu wengi amesema posta ndio chombo pekee cha kuelimika kwa kupata habari kuhusu afya na usalama.
Pia amesema katika enzi ya sasa ya kidigitali, Posta imejiweka katika nafasi ya mchangiaji mkuukwenye ulimwengu wa biashara ya mtandao yaani e-commerce.
Kauli mbiu yam waka huu ni ‘Posta hutoa hutoa huduma bora kwa dunia”.
UPU iliundwa mwaka 1874 na makao yake makuu yako Berne Uswisi. Na ndiyo shirika lisilo la kiserikali kongwe zaidi duniani na limekuwa chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1948. Duniani kote kuna wafanyakazi wa Posta wapatao milioni tano, na ofisi 663,000 katika nchi 192.