Washona kutoka Zimbabwe wafurahia baada ya watoto wao 600 kupatiwa utaifa Kenya

7 Agosti 2019

Nchini Kenya zaidi ya watoto 600 ambao walikuwa hawana utaifa kwa sababu wazazi wao walikuwa ni kabila la washona kutoka Zimbabwe,  sasa wamepatiwa vyeti vya kuzaliwa na hivyo kuwafungulia njia ya kupata huduma za msingi kama watoto wengine. Arnold Kayanda na taarifa zaidi.

Jijini Nairobi, Kenya shamrashamra zikitamalaki kutoka kwa wazazi wa kabila la washona wa nchini Zimbabwe baada ya serikali ya Kenya kuamua kuwapatia watoto wao vyeti vya kuzaliwa.

Washona hawa waliwasili Kenya wakitokea Zimbabwe miaka ya 1960 wakieneza dini wakiwa na hati za kusafiria za iliyokuwa Rhodesia na walisajiliwa kama vijakazi wa waingereza.

Hata hivyo baada  ya uhuru wa Kenya mwaka 1963 hawakuwa na kitambulisho cha utaifa na hivyo walisalia bila utaifa wakikosa huduma za msingi kama vile elimu na bima ya afya n ahata hakuweza kusafiri au kumiliki mali.

Watoto wao wakiitwa mmoja baada ya mwingine, mmoja wa wazazi ni Emma Muguni, mama wa watoto sita.

“Mambo yatabadilika. Ukiwa na hii nyaraka, wanaweza kutembea pahala popote na wanaweza kujiendeleza kimaisha. Yaani kutembea tu na nyaraka hii kutasaidia.”

Hatua hii imepongezwa na ni mwelekeo sahihi wa kuwapatia utaita washona 3,500 wenye umri wa chini ya miaka 18, George Kegoro ni Mkurugenzi Mtendaji tume ya haki za binadamu Kenya. “suala kwamba jamii kubwa haina utaifa, linadumaza malengo yote ya kijamii. Huwezi kufikia malengo iwapo baadhi ya wanajamii hawana uwezo wa kuyafikia eti tu kwa sababu hawana utaifa. Mfano huwezi kufikia lengo la huduma ya afya kwa wote kwa sababu ya tatizo lao la utaifa. Nadhani sasa kuna azma ya dhati ya serikali na haipotezi kitu kwa kuwapatia utaifa wasio na utaifa ambao wanaishi kwenye ardhi ya Kenya. Yenyewe itanufaika zaidi.”

Hi si mara ya kwanza kwa Kenya kuwapatia utaifa raia wa kigeni, kwa kuwa mwezi Oktoba mwaka 2017,  watu 6000 wenye asili ya Kimakonde waliondokana na tatizo la kutokuwa na utaifa baada ya serikali ya Kenya kuwatambua na kuwapa vitambulisho.

 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii