Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wapitisha rasmi mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi

Maria Fernanda Espinosa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akitoa hotuba katika uzinduzi rasmi wa mkataba kuhusu wakimbizi. "Kielelezo cha mshikamano na ushirika."
UN Photo/Mark Garten)
Maria Fernanda Espinosa, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akitoa hotuba katika uzinduzi rasmi wa mkataba kuhusu wakimbizi. "Kielelezo cha mshikamano na ushirika."

Umoja wa Mataifa wapitisha rasmi mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Mamilioni ya watu kote duniani hutumia miaka mingi ya maisha yao ukimbizini na wengine wakihatarisha maisha yao katika harakati za kusaka usalama wakienda wasikokujua. Amesema hayo leo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi Amina J. Mohammed, wakati wa hafla ya kupitisha rasmi mkataba mpya wa wakimbizi, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani. 

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Bi. Mohammed amesemma,

“Kwa muda mrefu mataifa ambayo yako karibu na maeneo yenye migogoro yamekuwa yakiwahifadhi wakimbizi wengi licha ya kuwa na matatizo yao ya kiuchumi. Mfano katika bonde la ziwa Chad watu maskini kabisa duniani walifungua milango ya nyumba zao kuwakaribisha watu wanaokimbia wapiganaji wa Boko Haram.Ukaribu kama huo hauko mahali pote.Ni majuzi tu tumeshudia kufungwa kwa mipaka kinyume na sheria za kimataifa kuhusu wakimbizi na haki za kibinadamu.”

Ameongeza kuwa ndio sababu mkataba huu ni hatua moja muhimu na endapo wote tutashikamana basi tunaweza  kufanikisha uwezo wake kuwalinda vyema na kuwasaidia  wakimbizi na  nchi zinazowapa hifadhi.

 

Katika picha hii ya maktaba tunaona wakimbizi wa Burundi wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wakisubiri kwenye ufukwe wa ziwa Tanganyika ili wasafirishwe kwa boti kwenda kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma nchini Tanzania. Huduma sasa zinasuasua.
UNHCR/B. Loyseau
Katika picha hii ya maktaba tunaona wakimbizi wa Burundi wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wakisubiri kwenye ufukwe wa ziwa Tanganyika ili wasafirishwe kwa boti kwenda kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma nchini Tanzania. Huduma sasa zinasuasua.

Kwa upande wake Kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudimia wakimbizi ,UNHCR, Filippo Grandi ambaye kwa kipindi cha miaka 30 aliyofanya kazi, muda wake mwingi ameutumia katika masuala ya wakimbizi anasema hatua ya leo ni ya kihistoria kwa sababu,

“Hii ndiyo mara ya kwanza naona  juhudi za pamoja ambazo ni za wazi za kitaasisi na pana, kuweza kuleta maana kuhusu kile kilichoainishwa katika mkataba kwamba wakimbizi kwamba suala la wakimbizi ni jukumu la jamii ya kimataifa. Hii ni kuleta maana ya wazo kwamba huu ni wajibu ambao sote tunahusika.”

Miongoni mwa waliopaza sauti zao pia ni  mkimbizi kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC aliyebahatika kupewa fursa ya kuishi Marekani kupitia mpango wa UNHCR wa kuwahamishia wakimbizi katika taifa la tatu . Bertine Bahige, anasema mbali na kupewa mahali pa kulala na kula kambini,  jambo analolifurahia zaidi ni kupewa nafasi ya kujiendeleza kielimu

“Moja ya matamanio niliyonayo na niliyokuwa nayo kabla,ilikuwa ni  kupata elimu na kupata uwezo wa kuanza kujenga maisha yangu na kuendelea kuyajenga bila kujali kile kilichoko mbele yangu,kwa sababu hilo linaniwezesha kuchangia katika  jamii niliyomo.”

Elsie Nzeyimana kutoka Burundi na anaishi Maine nchini Marekani.Yeye ni moja wa wanakwaya ya wakimbizi inayoitwa, Pinhcintu Refugee Youth Choir ambayo imeimba wakati wa uzinduzi wa mkataba kuhusu wakimbizi.
ONU Info/Florence Westergard
Elsie Nzeyimana kutoka Burundi na anaishi Maine nchini Marekani.Yeye ni moja wa wanakwaya ya wakimbizi inayoitwa, Pinhcintu Refugee Youth Choir ambayo imeimba wakati wa uzinduzi wa mkataba kuhusu wakimbizi.

Awali rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Maria Fernanda Espinosa alisisitiza kuwa leo ni siku nzuri kwa ulimwengu,na pia

Ni siku nzuri kwa wakimbizi milioni 25 duniani kote, na ni siku nzuri kwa jamii na mataifa yanayowahifadhi wakimbizi ambao sasa watapata msaada zaidi unaohitajika, na ni siku nzuri kwa baraza kuu la Umoja wa Mataifa ambalo limedhihirisha kwa mara nyingine tena,kuwa la umuhimu, katika kushughulikia changamoto za kimataifa na kwa kuidhinisha mkataba wa wakimbizi hii leo.”

Mkataba huu umepitishwa kwa madhumuni ya kuwezesha kuwa na mfumo mzuri na wenye mpangilio ili kuboresha maisha ya wakimbizi na jamii zinazowahifadhi kufuatia miaka miwili ya majadiliano ya kina ambayo yanafahamika kwa kila  aliyefuatilia mwelekeo wa Mkataba wa kimataifa wa  Uhamiaji salama, wenye mpangilio na ulio wa kawaida uliopitishwa Marrakech nchini Morocco Jumatatu iliyopita.