Elimu, ujumuishwaji na mabadiliko ya tabianchi ni baadhi vya vipaumbele vya Kenya:rais Kenyatta

26 Septemba 2019

Tumefika hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuungana na nchi wanachama kuelezea ambayo Kenya imeyafanya katika kuhakikisha inaendana na vipaumbele vya mkutano huu wa Baraza Kuu la Umoja huo UNGA74 ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, ujumuishwaji na ushirikiano wa kuhakisha utimizaji wa malengo ya maendeleo endelevu SDGs ifikapo mwaka 2030.

Hiyo ni kauli ya rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika mahojiano nami punde baada ya kuwasilisha hotuba yake kwenye mkutano wa Baraza Kuu unaoendelea jijini New York, Marekani ambapo amesema kwa kuzingatia hayo, "mambo hayo ndio yatatusaidia kuhakikisha ya kwamba tumemaliza umaskini, tumepambana na maswala ya mabadiliko ya tabianchi, tumesomesha watoto, tumezingatia mazingira na tumehakikisha ya kwamba hakuna yeyote atakaye achwa nyuma katika ajenda ya mwaka 2030 na njia pekee ni kwa kushirikiana kufanya kazi pamoja, alafu nimefafanua pia yale nchini Kenya tumefanya na tunayoyafanya katika kutimiza ahadi za mwaka 2030 ambazo wote tuliridhia."

Rais Kenyatta alienda mbali zaidi kuelezea ni masuala yapi ambayo wameyapatia kipaumbele ambapo amesema, "kwanza ni masomo, kuhakikisha kwamba watoto wetu wataweza kusoma kutoka darasa la kwanza na kumaliza hadi kidato cha nne, hapo awali tulikuwa tunatoa elimu bila malipo kwa wanafunzi kuanzia darasa la kwanza hali la nane lakini kwa sasa tunatoa elimu hyo bila malipo kwa wanafunzi wa hadi kidato cha nne ambao wako shule ya kutwa watagharamiwa na serikali ili kuhakikisha kwamba kila kijana aliye chini ya umri wa miaka 18 yuko shuleni na baada ya hapo anakwenda chuo kikuu au taasisi za stadi."

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter