Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yafikia rekodi mpya ya watu milioni 12.4 na msaada wa chakula nchini Yemen

Mfanyakazi wa WFP akiangalia Lori lililoleta msaada wa chakula katika kambi ya Khudais Yemen mwezi Juni 2019
WFP/Mohammed Awadh
Mfanyakazi wa WFP akiangalia Lori lililoleta msaada wa chakula katika kambi ya Khudais Yemen mwezi Juni 2019

WFP yafikia rekodi mpya ya watu milioni 12.4 na msaada wa chakula nchini Yemen

Msaada wa Kibinadamu

Takwimu mpya kufuatia shughuli ya mgao wa chakula mwezi Agosti zinaonyesha kuwa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP, lilifikia rekodi mpya kufikishia chakula  watu milioni 12.4, wanaokumbwa na uhaba wa chakula  mwezi Agosti.

Hii ndio idadi kubwa zaidi kuwai kufikiwa, amesema Herve Verhoosel, msemaji wa WFP akiongeza kuwa kuagizwa chakula, kukihifadhi na kukisafirisha kuwalisha zaidi ya watu milioni 12 kwa mwezi katika eneo la vita, ni wajibu ulio mkubwa.

“Kufanikisha hili, tunahitajia kuhakikisha uwepo wa chakula usiokoma kwenda nchi hiyo. Kusistisha usafirishaji wa chakula inahujumu uwezo wetu wa kutoa msaada huu, amesema Verhoosel.

Hata hivyo amesema WFP inahitaji dola milioni 600 kuhakikisha kuwa watu wanapata chakula bila tatizo katika kipindi cha miezi sita hadi Februari mwaka 2020.

Verhoosel  amesema kuwa bila ya ufadhili zaidi WFP haitakuwa na uamuzi mwingine bali itapunguza chakula kwa familia kuanzia mwezi ujao wa Oktoba. “Tunahitaji kuwa na chakula kinachoingia Yemen kila mara", amesisitiza Verhoosel.

Amekumbusha kuwa "Huku kukiwa na watu milioni 20.1 wanaokumbwa na uhaba wa chakula kati ya jumla ya watu wote milioni 30 nchini Yemen, ni lazima tuhakikishe kuwa kwa kila mwezi WFP inaweza kutoa msaada unaosubiriwa sana na mamilioni ya watu wenye njaa."