Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP ‘yasitisha’ mgao wa chakula kwenye maeneo yanayodhibitiwa na wahouthi Sana’a

Mtoto akiwa na utapiamlo anapata matibabu katika hospitali ya Al Sabeen mjini Sana'a, Yemen.
WFP/Marco Frattini
Mtoto akiwa na utapiamlo anapata matibabu katika hospitali ya Al Sabeen mjini Sana'a, Yemen.

WFP ‘yasitisha’ mgao wa chakula kwenye maeneo yanayodhibitiwa na wahouthi Sana’a

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limethibitisha hii leo kusitisha kwa kiwango kidogo mgao wa chakula kwenye maeneo yanayodhibitiwa na majeshi ya upinzani ya wahouthi nchini Yemen.

Msemaji wa WFP mjini Geneva, Uswisi, Hervé Verhoosel amewaeleza waandishi wa habari kuwa uamuzi wa shirika hilo umechukuliwa baada ya kushindikana kwa juhudi za kuepusha misaada kwenda kwa wasiohusika.

“Katika maeneo  yoyote ya mizozo, baadhi ya watu wanasaka kujinufaisha na kuhangaika kwa wengine na kupeleka chakula cha msaada kwa wasiohusika. WFP imekuwa ikisaka msaada kutoka kwa mamlaka kwenye mji mkuu wa Yemen, Sana’a ili kuweza kupata mfumo wa kupata vitambulisho vya kutumia viungo vya mwili.”

Bwana Verhoosel amesema mfumo wa aina hiyo ungesaidia kulinda familia za wayemen na kuhakikisha chakula kinawafikia wale wanaohitaji zaidi, “bahati mbaya makubaliano yameshindwa kufikiwa.”

Uamuzi huu wa karibuni zaidi una maana kwamba msaada kwa wahitaji huko Sana’a kunakodhibitiwa na wahouthi, utasitishwa na hivyo kuathiri watu 850,000, ingawa Bwana  Verhoosel amesisitiza kuwa shirika hilo litaendelea na miradi ya kugawa chakula cha lishe kwa watoto na wajawazito na wanawake wanaonyonyesha.

Kwa mujibu wa makadirio ya WFP, watu milioni 9 kati ya watu milioni 12 wanaohitaji msaada wa chakula nchini Yemen wako kwenye maeneo  yanayodhibitiwa na wahouthi.

Kwa zaidi ya miaka minne sasa, wahouthi wamekuwa wakipigana dhidi ya vikosi vinavyomuunga mkono Rais Abrdabbuh Mansour Hadi.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa takribani watu milioni 10 nchini Yemen hawana kabisa chakula na hawafahamu watapata wapi mlo wa kesho.