Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maoni ya wakuu wa nchi yanaweza kutofautiana lakini yakatatua changamoto zinazoikabili dunia-Balozi Modest Mero

Balozi Modest Mero, mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa wakati wa mahojiano na Idhaa ya Kiswahili.
UNnewskiswahili/Patrick Newman
Balozi Modest Mero, mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa wakati wa mahojiano na Idhaa ya Kiswahili.

Maoni ya wakuu wa nchi yanaweza kutofautiana lakini yakatatua changamoto zinazoikabili dunia-Balozi Modest Mero

Masuala ya UM

Tukielekea wiki ya vikao vya mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa vitakavyowakutanisha viongozi wa dunia katika makao makuu ya umoja  huo mjini New York Marekani kuanzia jumatatu ya wiki ijayo, Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Modest Mero amezungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa na kueleza kuwa mijadala ya viongozi wakuu wa dunia itatawaliwa na changamoto kuu tano ambazo dunia nzima inakabiliana nazo hivi sasa.

Balozi Mero amesema kuwa, “huu ni mkutano muhimu sana katika miaka yote ambayo mimi nimekuwa hapa katika Umoja wa mataifa. Kwanza kabisa tunaangalia maendeleo ya watu na changamoto ambazo wanakumbana nazo. Kuna changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa, kuna changamoto za afya ya watu, kuna changamoto pia za maendeleo yao ambayo yako kwenye maeneo ya maendeleo endelevu, kuna matatizo pia ya namna ya kutoa fedha za ufadhili katika kuleta maendeleo hayo hayo tunayoyazungumzia. Lakini ya mwisho tutavizungumzia zaidi visiwa vidogo vidogo ambavyo mataifa yake yako hatarini kutoweka duniani akama hatutachukua hatua hasa kwenye upande wa mabadiliko ya hali ya hewa”

Na kuhusu ni kwa namna gani mataifa yanaweza kufikia maamuzi ya pamoja katika masuala mazito kama hayo, Balozi Mero anasema, “hayo masuala matano yatajadiliwa kutegemeana  na namna ambavyo mjadala utakavyojitokeza. Inawezekana kabisa watakaoshiriki wakiwa ni wakuu wa hizi nchi wakawa na maoni tofauti  lakini yakawa yanaelekea mahali pamoja tu ambako ni kutatua haya matatizo   na kufanya hali za wananchi wao n anchi zao kuwa bora zaidi kuliko hivi sasa au kuweka mikakati ya kuzuia changamoto hizo zisiendelee kujitokeza katika nchi zao.”