Kutowashirikisha vijana kwenye tabianchi ni janga- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa katika mahojiano maalumu na Mkuu wa Idara ya mawasiliano ya umma ya Umoja wa Mataifa Melissa Fleming mjini New York Marekani Septemba 18, 2019.
UN News/Ben Lybrand
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa katika mahojiano maalumu na Mkuu wa Idara ya mawasiliano ya umma ya Umoja wa Mataifa Melissa Fleming mjini New York Marekani Septemba 18, 2019.

Kutowashirikisha vijana kwenye tabianchi ni janga- Guterres

Masuala ya UM

Kuelekea siku ya kimataifa ya amani ambayo huadhimishwa kila mwaka Septemba 21, leo katika maadhimisho kwenye Umoja wa Mataifa Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Guterres ametoa wito wa hatua madhubuti kuchukuliwa kukabiliana na changamoto kubwa za dunia ikiwemo mabadiliko ya tabianchi ili kudumisha amani kwa wote. 

Akihimiza hatua Madhubuti kuhakikisha amani katika tukio la leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku ya amani likiambatana na burudani na kengele ya amani Guterres amesema ni jukumu la kila mtu kuitetea na kuilinda amani tuliyonayo kwa kutekeleza wajibu wao.

Aidha mapema akihojiwa na Melissa Fleming,  Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma ya Umoja wa Mataifa,  na Bwana Guterres amesema katika mchakato wa kukabiliana na changamoto hizo, ni muhimu kuwashirikisha vijana katika kila maamuzi yanayofanyika hivi sasa kwani katika miongo michache ya ijayo ndio watakaokuwa wanakabiliana na matatizo yatakayotokana na makosa yanayoweza kufanyika wakati wa sasa.

Katibu Mkuu Guterres ameyasema hayo pale ambapo  Bi Fleming  alitaka kufahamu umuhimu wa mkutano wa vijana kuhusu tabianchi, mkutano utakaofanyika mwishoni mwa juma hili mjini New York Marekani.

Bwana Guterres amesema ni muhimu kwa kuwa vijana wameonesha uongozi mkubwa katika suala hilo na inaeleweka kikamilifu mabadiliko ya tabianchi tayari ni shida kubwa hivi sasa na ni wazi kuwa itakuwa shida kubwa zaidi katika miaka ijayo.

Amesema ni kwa mantiki hiyo vijana wa leo watakuwa watu wazima watakaoiongoza dunia katika miongo michache ijayo akisema,“na kwa hivyo vijana wamekuwa kabisa mstari wa mbele katika kuzishinikiza serikali na kushinikiza biashara, miji na wadau wengine wote kufanya yale wanayopaswa kufanya kudhibiti mabadiliko ya tabiachi. Kwa hivyo mkutano wa vijana ni muhimu sana ili kuweka msukumo kwa wale wanaotakiwa kufanya maamuzi.”

Alipoulizwa matumaini yake kuhusu amani na usalama, Guterres amesema kuna mweleleo chanya Sudan, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya kati, na kuwa uchaguzi ambao ulitegemewa kuwa na matatizo kama vile wa DRC, Maldives na Madagascar ulikamilika bila vurugu, lakini anaongeza,“kwa hivyo kuna dalili nyingi chanya, lakini bahati mbaya tuna dalili nyingine hasi na tunaona watu watu wakifa nchini Syria, Libya na Yemen. Na kwa hivyo tunahitaji kuongeza ahadi yetu kwa ajili ya amani na tuzifanye nchi zielewe na hususani wale ambao kwa kiasi fulani wanawajibika na vita hizi kuwa hakuna anayeshinda, kila mtu anashindwa.”

Na kuhusu ujumbe wake kwa viongozi wa dunia ambao watakuna katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa wiki ijayo, Katibu Mkuu Guterres anawasihi kufanya kila kinachohita ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na uwezo wa kutatua shida ambazo wanadamu wanakabiliana nazo.