Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajumbe wapya wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la UN watangazwa

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ( Maktaba)
UN photo /Loey Felipe
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ( Maktaba)

Wajumbe wapya wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la UN watangazwa

Masuala ya UM

Algeria, Guyana, Jamhuri ya Korea, Sierra Leone na Slovenia kwa muda wa miaka miwili, kuanzia mwezi Januari 2024 zitaungana na wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kudumisha amani na usalama wa kimataifa.

Nchi tano HIZO zimechaguliwa kuwa wajumbe wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia upigaji kura katika Baraza Kuu leo Jumanne katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Nchi hizi zilikuwa miongoni mwa nchi sita zilizowania viti vitano visivyo vya kudumu kwenye meza ya Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kupata kiti

Baraza la Usalama linaundwa na nchi 15, tano kati yake ni wajumbe wa kudumu ambao ni China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani  na wana haki ya kupiga kura ya turufu dhidi ya uamuzi wowote.

Wanachama 10 wasio wa kudumu wanachaguliwa na Baraza Kuu, ambalo linajumuisha Nchi Wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa, na moja ya mambo yanayozingatiwa ni mgawanyo wa kijiografia.

Upigaji kura unafanywa kwa kura ya siri na wagombea lazima wapate wingi wa theluthi mbili, au kura 128, hata kama watashiriki bila kupingwa.

Kwa ujumla, nchi 192 zilipiga kura kujaza viti vitatu vya Baraza vilivyotengwa kwa Makundi ya Afrika na Asia-Pasifiki, na kimojakimoja kwa ajili ya Ulaya Mashariki na Amerika Kusini na Karibea.

Slovenia imeishinda Belarus katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya Ulaya Mashariki kwa kupata kura 153 dhidi ya 38, huku Algeria, Guyana, Sierra Leone na Jamhuri ya Korea zikipita bila kupingwa.

Tayari kuhudumia

Nchi tano zilizochaguliwa zitaungana na Ecuador, Japan, Malta, Msumbiji na Uswisi kama wajumbe wasio wa kudumu wa Baraza.

Wajumbe hawa wapya wanachukua viti vinavyokaliwa kwa sasa na Albania, Brazil, Gabon, Ghana na Falme za Kiarabu wakati mihula yao ya miaka miwili itakapokamilika tarehe 31 Disemba mwaka huu 2023.