Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi 41 zahitaji msaada wa chakula, idadi kubwa zinatoka Afrika- FAO

Kilimo barani Afrika kinapaswa kuangaziwa upya ili kisiwe chanzo cha kudorora kwa uchumi
FAO/Alessandro Stelzer
Kilimo barani Afrika kinapaswa kuangaziwa upya ili kisiwe chanzo cha kudorora kwa uchumi

Nchi 41 zahitaji msaada wa chakula, idadi kubwa zinatoka Afrika- FAO

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema takribani mataifa 41 yanaendelea kuhitaji msaada wa chakula kutoka nje, sababu kuu ikiwa ni mizozo na hali mbaya ya hewa.

FAO kupitia ripoti yake inayotolewa kila robo mwaka kuhusu matarajio ya mazao na hali ya chakula imesema kati ya nchi hizo 41, 31 ni kutoka Afrika zikiwemo Burundi, Uganda, Zimbabwe, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan, Liberia,Niger,Senegal, Sierra Leone, Mauritania, na Msumbiji.

Ikiwa imetolewa leo huko mjini Roma, Italia, ripoti hiyoi inasema mizozo na ukosefu wa usalama vimechochea ukosefu wa uhakika wa chakula nchini Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na baadhi ya maeneo ya Nigeria.

Hata hivyo uhaba wa mvua hasa kwenye maeneo ya  nchi za Afrika Mashariki umechochea ukosefu wa chakula ikielezwa kuwa kwa ujumla uzalishaji wa nafaka kwa mwaka 2019 kwenye ukanda huo unatarajiwa kupungua kwa asilimia 5.6 kutoka kiwango cha mwaka jana.

Ripoti hiyo inasema anguko kubwa la uzalishaji wa nafaka linatarajiwa katika nchi za Kenya na Sudan huku bei za mazao kama vile mahindi na mtama zikiwa zimeongezeka kwa kiwango kikubwa na uhakika wa chakula ukipungua kwa kiasi kikubwa Kenya na Somalia.

Hali mbaya ya hewa imepunguza kwa asilimia 50 uzalishaji wa wa mazao nchini Zimbabwe kwa mwaka huu wa 2019 huku idadi ya watu wasio na uhakika wa chakula nchini humo ikitarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwakani.

Mataifa mengine kando ya Afrika yanayokabiliwa na uhaba wa chakula na hivyo kulazimika kupata msaada kni Yemen, Syria, Venezuela, Korea Kaskazini na Pakistani.

Nchini Korea Kaskazini, FAO inasema kuwa uzalishaji wa mazao unatarjiwa kuwa wa chini kuliko kawadai kutokana na kiwango kidogo cha mvua na kiwango kidogo cha maji ya umwagiliaji katika awamu ya pili ya mwaka huu wa 2019.

Kutokana na hali hiyo, asilimia 40 ya wananchi wa Korea Kusini watakuwa hawana uhakika wa kupata chakula na hivyo kuhitaji msaada dharura.