Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uzalishaji wa sukari India na Brazil waporomosha bei ya sukari duniani-FAO

Uzalishaji wa tambi huko Parma nchini Italia katika picha hii ya t arehe 3 Oktoba 2012. Tambi ni moja ya vyakula vitokanavyo na nafaka.
FAO/Alessia Pierdomenico
Uzalishaji wa tambi huko Parma nchini Italia katika picha hii ya t arehe 3 Oktoba 2012. Tambi ni moja ya vyakula vitokanavyo na nafaka.

Uzalishaji wa sukari India na Brazil waporomosha bei ya sukari duniani-FAO

Masuala ya UM

Bei za vyakula duniani kwa mwezi uliopita wa Disemba hazikubadilika ambapo ongezeko la bei nafaka lilipatiwa uwiano na kupungua kwa bei ya sukari na bidhaa za maziwa, limesema shirika la chakula na kilimo duniani hii leo, FAO.

FAO inasema kipimo cha bei kwa Disemba kilikuwa wastani wa pointi 161.7 ikilinganishwa na kipimo cha 161.6  mwezi uliotangulia wa Novemba na hivyo kutokuwepo na tofauti kubwa.

Kwa mujibu wa FAO, kipimo hicho kinatumika kama kiashiria cha mabadiliko ya bei za chakula kimataifa ambapo kwa wastani mwaka 2018 kilikuwa pointi 168.4 ikiwa ni pungufu kwa asilimia 3.5 ikilinganishwa na mwaka 2017 na chini zaidi kwa asilimia 27 mwaka 2011.

Bei ya sukari ndio inaonekana iliporomoka zaidi  kwa wastani wa asilimia 22 mwaka 2018 ikilinganishwa na mwaka 2017.

Sababu ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa sukari nchini India na Brazil sambamba na kuporomoka kwa bei ya mafuta ghafi hali iliyochochea kupungua kwa mahitaij ya miwa katika kuzalisha Ethanol.

Bei ya mahindi iliongezeka kidogo kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa upande wa kaskazini mwa dunia ilhali mchele uliporomoka bei kwa miezi sita mfululizo.