Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umaskini, elimu na ujumuishaji ni vipaumbele vya kwanza katika orodha ya vipaumbele vya Rais mpya wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Balozi Tijjani Muhammad-Bande, Rais mteule wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akizungumza na vyombo vya habari vya Umoja wa Mataifa
UN News/Nam Cho
Balozi Tijjani Muhammad-Bande, Rais mteule wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akizungumza na vyombo vya habari vya Umoja wa Mataifa

Umaskini, elimu na ujumuishaji ni vipaumbele vya kwanza katika orodha ya vipaumbele vya Rais mpya wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Masuala ya UM

Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ukianza rasmi leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Rais mteule wa mkutano huo Balozi Tijjani Muhammad-Bande ametaja vipaumbele vyake vitatu kuwa ni umaskini, elimu bora na ujumuishaji wa kila mtu. 

Balozi Tijjani ambaye ni mwakilishi wa kudumu wa Nigeria katika Umoja wa Mataifa ameyaeleza hayo katika mahojiano yake ya kwanza na vyombo vya habari vya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani tangu alipochaguliwa mnamo mwezi Juni mwaka huu wa 2019 kusimamia mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoanza leo na utamalizika mwezi Septemba mwakani.

Balozi Tijjani anasema kando na vipaumbele vile vya kawaida vya marais wote wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ukiacha amani na usalama, ambayo ni muhimu, vingine vitatu ni,

(Sauti ya Tijjani)

Rais wa Baraza Kuu kikao cha 74- balozi Mohammed Bande

“Vipaumbele vyangu vitatu ni kutokomeza umaskini, elimu bora na ujumuishwaji.”

Balozi Tijjani ambaye ni mtaalamu wa sayansi ya siasa kutoka chuo kikuu cha Ahmadu Bello, Nigeria, akiwa amejipatia pia shahada ya uzamili nchini Marekani katika Chuo kikuu cha Boston na pia shahada ya uzamivu katika  Chuo Kikuu cha Toronto Canada, anasisitiza kwa nini kwake elimu ni kipaumbele, akisema, "elimu ni jambo tete. Yeyote ambaye amenyimwa elimu ni kama amenyimwa kila kitu. Tukiwa na elimu, tunaweza kuwa na chuki kidogo, tunaweza kuwa na uelewano bora. Tunaweza kuwa na usawa zaidi.”

Akijibu swali la Umoja wa Mataifa unasimama wapi ukitimiza miaka 75 mwakani tangu kuanzishwa kwake, Balozi Tijjani Muhammad-Bande anasema,

(Sauti ya Tijjani)

“Ni wakati muhimu. Na unapaswa kutukumbusha kuhusu madhumuni ya shirika hili, na ahadi zake, na ahadi zake hizi ndizo tunatakiwa kukumbuka wakati wote.”