Mtaalam wa UN kutathimini hali ya haki za uhuru wa kuandamana na kujumuika Zimbabwe

12 Septemba 2019

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa Clément Nyaletsossi Voule atatembelea Zimbabwe kuanzia tarehe 17 hadi 27 mwezi huu wa Septemba 2019 kwa ajili ya kutathimini hali na changamoto ya haki za uhuru wa kuandamana kwa amani na kujumuika nchini humo.

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, imesema hii ni ziara ya kwanza rasmi ya kiofisi inayofanywa chini Zimbabwe na mtaalamu huru wa haki za binadamu aliyeteuliwa na baraza la haki za binadamu.

“Ziara yangu hii nchini Zimbabwe inawakilisha fursa muhimu kujifunza kuhusu sheria, sera na hali halisi ya kitaifa kuhusiana na haki za kuandamana na kukusanyika kwa amani kulingana na katiba ya mwaika 2013 na mabadiliko ya uongozi.” Amesema Voule.

“Mpango wangu pia utasaidia kutambua fursa na changamoto ambazo serikali inakabiliana nazo katika kutekeleza kifungu cha 21 na 22 vya mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa hususani kuhusianisha na mikusanyiko katika muktadha wa maandamano ya hivi karibuni.” Amefafanua Bwana Voule.

Mtaalamu huyo ambaye anaitembelea Zimbabwe kwa mwaliko wa serikali ya nchi hiyo, atakutana na maafisa wa serikali, wawakilishi wa mahakama, bunge, taasisi huru na jumuiya za kiraia. Atakutana pia na wajumbe wa jumuiya ya kimataifa wakiwemo maafisa wa Umoja wa Mataifa.

Wakati wa ziara yake hiyo ya siku kumi, Bwana Voule anatarajiwa kutembelea jamii katika maeneo ya Bulawayo, Mutare na Marange.

Mara baada ya ziara hiyo, mtaalamu huyo ataeleza sehemu ya awali ya awali ya uchunguzi wake katika mkutano wa wanahabari tarehe 27 Septemba mwaka huu mjini Harare katika jengo la Sanders, ghorofa ya pili, kisha atawasilisha ripoti kamili itakayojumuisha na ushauri katika kikao cha 44 cha baraza la haki la haki za binadamu mwezi Juni 2020.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter