Sera nchini Zimbabwe zawaweka taabani zaidi walalahoi- Wataalamu

4 Aprili 2019

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wameonya kuwa sera zinazotekelezwa nchini Zimbabwe zinazidi siyo tu kudororesha uchumi wa nchi bali pia zinafanya hali kuwa mbaya zaidi kwa walala hoi na wale wanaopaza sauti kulalamika.
 

“Tuna wasiwasi mkubwa sana na hali hiyo kadri hali inavyozidi kuzorota nchini Zimbabwe, serikali inazidi kusongesha watu kwenye umaskini,” wamesema wataalamu hao leo kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR.

Wataalamu wamesema wana hofu kwa kuwa hawana taarifa iwapo kuna hatua zozote za serikali za kuwapatia walala hoi kiwango hata kidogo cha fedha cha kujinusuru hasa wale ambao tayari maisha wanayoishi ni ya kifukakara kutokana na sera za sasa za kiuchumi.
 
“Madhara ya marekebisho ya kiuchumi kwenye haki za binadamu lazima yatathminiwe kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na maadili sambamba na misingi ya haki za binadamu,” wamesema wataalamu hao.
 
Mfano wa sera hizo ni tangazo la serikali ya Zimbabwe la kuonyesha nia yake ya kukata kwa asilimia 50 matumizi yake ikiwa ni njia ya kukabiliana na janga litokanalo na usimamizi mbovu wa uchumi.

Wataalamu hao wamesema hawana uhakika ni kwa vipi madhara yatokanayo na hatua hiyo yatakumba watu wote yaani maskini na tajiri ikizingatiwa kuwa walio nacho wanalindwa na kampuni za fedha, ilhali maskini watakumbwa na bei za juu za bidhaa na viwango vya juu vya kodi.
 
Bei za bidha ani pamoja na ongezeko la bei ya petroli lililotangazwa na Rais tarehe 12 Januari 2019, ambapo bei imeongezeka maradufu na kuwa bei ya juu zaidi duniani.
Hatua hiyo imesababisha bei ya vyakula na usafirishaji kuongezeka maradufu.
 
Tayari mashirika ya haki za binadamu yameonya kuwa Zimbabwe inaweza kukumbwa na janga la kibinadamu na hivyo wataalamu wa haki za binadamu wametaka serikali izingatie mikataba ya haki za binadamu ambayo imeridhia ili kulinda wananchi wake.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud