Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Angola yapokea msaada wa UNCTAD kupiga jeki uchumi na kilimo

Jimbo la Cunene nchini Angola
© UNICEF Angola/2019/Carlos Louzada
Jimbo la Cunene nchini Angola

Angola yapokea msaada wa UNCTAD kupiga jeki uchumi na kilimo

Msaada wa Kibinadamu

Serikali ya Angola imepokea msaada kutoka kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa UNCTAD, kwa ajili ya mabadiliko ya mazingira ya biashara kwa lengo la kuinua uchumi na kuwekeza katika kilimo.

Wizara za biashara na uchumi na mipango za nchi hiyo zimekutana na kamati ya UNCTAD na kujadili mabadiliko yatakayosaidia kuinua uwekezaji wa nje kwa ajili ya kupanua wigo wa uchumi wakati wa uwasilishaji wa tathimini ya sera ya uwekezaji kwenye warsha ya kitaifa  iliyofanyika nchini Angola mwishoni mwa wiki na kushirikisha pia umma na sekta binafsi.

Akisisitiza kuhusu malengo ya serikali katika mabadiliko ya uwekezaji na vipaumbele vyake Joffre Van-Dúnem waziri wa biashara wa Angola amesema “tathini ya sera za uwekezaji au IPR ni muhimu sana katika kuimarisha mazingira ya biashara, ikiwemo biashara ya kilimo.” Ameongeza kuwa baada ya kufikia hatua kubwa kufuatia kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe uwekezaji wa moja kwa moja toka nje, FDI umepungua katika miaka ya hivi karibuni, umekuwa tete na kujikita zaidi katika sekta ya uchukuzi. Amependekeza kuwa “wigo mpana zaidi wa miradi ya FDI unaokwenda sanjari na mahitaji ya waangola utafika mbali zaidi kwa kusaidia mafanikio ya malengo ya kitaifa ya maendeleo."

Ingawa serikali ya angola imeweka mkakati thabiti wa kitaifa wa mabadiliko ya mazingira ya biashara na uwekezaji, bado kuna mapengo na vikwazo chungu nzima ikiwemo mfumo tata kwa ajili mfumo na kanuni za FDI, hulka za biashara, na ukosefu wa uratibu na uwezo.

Na changamoto hizo zinaathiri uwezo wa nchi ya angola kutumia fursa ya eneo ilipo, rasilimali ilizonazo na fursa ya kupata masoko ya nje.

Nchini Angola, ukame unaathiri zaidi ya watu milioni 2.3 wakiwemo watoto 491,000 chini ya miaka mitano
© Unicef Angola/Carlos Louzada
Nchini Angola, ukame unaathiri zaidi ya watu milioni 2.3 wakiwemo watoto 491,000 chini ya miaka mitano

 

Kwa upande wake waziri wa uchumi na mipango Manuel Neto da Costa amesema “FDI ulikuwa ukipuuzwa na hali hii ilisababisha athari mbaya katika mzunguko wa kiuchumi na matatizo mengi tunayokabiliana mayo sasa yanashughulikiwa na IPR.”

Naye mkuu wa kitengo cha tathimini ya será za uwekezaji wa UNCTAD Bi. Chantal Dupasquier amesema “Angola itahitaji kukabiliana na mapengo makubwa na changamoto katika mazingira ya uwekezaji ili kufikia uwezo wake wa juu wa kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja toka nje, FDI.”

Warsha hiyo ya IPR imeendeshwa na UNCTAD kama sehemu ya mafunzo kwa ajili ya Trade II, ambao ni mradi wa miaka minne unaofadhiliwa na Muungano wa Ulaya. Lengo la mradi huo ni kusaidia nchi ya kuimarisha na kupanua wigo wa uchumi wake kabla yanchi hiyo kufuzu kutoka katika hadhi ya nchi zenye maendeleo duni hapo 2021.

UNCTAD imeshazisaidia zaidi ya nchi zinazoendelea 50 na chumi zao kufanya mabadiliko kwa kuendesha tathimini ya será zao katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Pia imetoa msaada wa kiufunzi katika utekelezaji wa mapendekezo ya IPR.