Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa kali yanyemelea kusini mwa Angola- WFP

Mtoto wa kike nchini Angola mwenye umri wa miaka miwili akila rojo lenye virutubisho vya lishe baada ya kubainika kuwa na utapiamlo
© WFP/Pedro Domingos
Mtoto wa kike nchini Angola mwenye umri wa miaka miwili akila rojo lenye virutubisho vya lishe baada ya kubainika kuwa na utapiamlo

Njaa kali yanyemelea kusini mwa Angola- WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP linaonya kuwa kiwango cha njaa kinazidi kuongezeka nchini Angola wakati huu ambapo taifa hilo la kusini mwa Afrika linakumbwa na ukame ambao haujawahi kushuhudiwa kwa miongo minne katika majimbo ya kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Msemaji wa WFP mjini Geneva, Uswisi Tomson Phiri amewaambia waandishi wa Habari kuwa hali ya hewa ya ukavu isiyo ya kawaida inakwamisha msimu wa mvua, ambao mara nyingi huanzia mwezi Aprili hadi Novemba. 

Amesema ukame umeshamiri nchini humo tangu mwezi Desemba mwaka jana na majimbo ya Cuanza Sul, Benguela, Huambo, Namibe na Huila kupata kiwango kidogo cha mvua na kwamba hali haitarajiwi kuwa bora hivi karibuni.

Bwana Phiri amesema kadri kiwango cha maji kinavyopungua, mazao yaanathirika na kuna uwezekano wa kupoteza hadi asilimia 40 ya mazao sambamba na hatari ya wananchi kushindwa kuendelea kutunza mifugo yao na sasa familia zinahamahama kuelekea majimbo mengine na nchi jirani ya Namibia.

Kwa hivi sasa WFP inaratibu tathmini za uhakika wa upatikanaji wa chakula na lishe kwenye maeneo hayo ya kusini mwa Angola, tathmini ambayo itapatikana mwishoni mwa mwezi wa Mei.

Shirika hilo limekuwa likisaidia serikali ya Angola kwenye maeneo ya mgao wa mlo shuleni, tathmini za hatari katika mwelekeo wa chakula na lishe na limesema litaendelea kufuatilia kwa karibu hali ilivyo na kutoa msaada wa kiufundi kwa kuzingatia mahitaji na mapengo yaliyopo.