Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi maskini zichagize ukuaji uchumi kufikia SDGs- UNCTAD

Biashara mtandao ni fursa kwa ajira. (Picha:UNCTAD/http://bit.ly/2hKAa4z)

Nchi maskini zichagize ukuaji uchumi kufikia SDGs- UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Kasi ukuaji uchumi kwa nchi maskini zaidi duniani inapaswa kuongezwa ili ziweze kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu mwaka 2030 ikiwemo kutokomeza umaskini.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya kamati ya maendeleo na biashara ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD iliyochapishwa hii leo.

Yaelezwa kuwa wastani wa ukuaji wa uchumi katika nchi hizo zilizopatiwa pia jina la LDCs ni asilimia 5 na ikiongozeka hadi asilimia 5.4 kwa mwaka.

Hata hivyo kiwango hicho ni kiduchu ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7 ambao umepangwa kwa mujbu wa lengo namba 8 la uchumi jumuishi, endelevu na shirikishi.

Paul Akiwumi, ambaye ni Mkurugenzi wa UNCTAD kanda ya Afrika, LDCs na miradi maalum amesema jamii ya kimataifa ni lazima iimarishe usaidizi wake kwa nchi hizo kwa mujibu wa azma mpya ya kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.

Amesema ukosefu wa usawa kati ya nchi maskini na zile tajiri unatishia kuongezeka kwa pengo hilo.

Ripoti hiyo ya uchambuzi imebainisha kuwa nchi hizo maskini zimesalia tegemezi kuuza nje bidhaa za kawaida na hilo ni lazima libadilishwe.