Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani ghasia dhidi ya wageni Afrika Kusini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
TASS/ UN DPI
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres

UN yalaani ghasia dhidi ya wageni Afrika Kusini

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vitendo vya ghasia dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini vinavyoenda sambamba na mashumbulizi dhidi ya raia wa kigeni pamoja na uharibifu wa mali.

Taarifa iliyotolewa hii leo jijini New York, Marekani na msemaji wa Umoja wa Mataifa, imemnukuu Katibu Mkuu akitambua kauli ya Rais Cyril Ramaphosa ya kulaani vikali vitendo hivyo na wito wake wa kutaka kuimarisha uwajibikaji kwa mujibu wa maadili ya Afrika Kusini yaliyoainishwa kwenye katiba.

Bwana Guterres ametoa wito kwa viongozi wote wa kisiasa kulaani na kukataa wazi wazi matumizi ya ghasia.

Vyombo vya habari vinaripoti ya kwamba ghasia hizo zinazozidi kushamiri kila uchao zimeshika kasi zaidi kwenye miji ya Pretoria na Johannesburg ambapo watu wapatao watano wameripotiwa kuuawa ilihali makumi kadhaa wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na fujo hizo.