Kinachosikitisha zaidi ubaguzi wa rangi na chuki vinaendelea: Guterres

20 Machi 2018

Mifumo yote ya ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni na kutovumiliana ni lazima iendelee kupingwa vikali kote duniani. Wito huo umetolewa leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, katika mjadala maalumu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kutokomeza ubaguzi wa rangi uliofanyika kwenye baraza kuu la umoja wa Mataifa mjini New York Marekani.

Katika siku hiyo ambayo kila mwaka huadhimishwa Machi 21, kuwaenzi watu 69 waliouawa kikatili wakiandamana kwa amani huko Sharpeville nchini Afrika Kusini kupinga ubaguzi wa rangi, Guterres amesema hali hiyo bado ipo na inaanza kumea mizizi kushika kasi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia Baraza Kuu kuhusu uhamiaji 01.11.2018 (maktaba). Picha: UM/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia Baraza Kuu kuhusu uhamiaji 01.11.2018 (maktaba). Picha: UM/Mark Garten

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

“Cha kusikitisha vitendo hivi bado vinaendelea katika nchi na miongoni mwa jamii kote duniani. Mfano mkubwa na wa kusikitisha ni jinsi wanavyotendewa ukatili  mabaya Waislamu wa jamii ya  Rohingya nchini Myanmar.”

Kwa mantiki hiyo amesisitiza

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

“Wakati umewadia kwa mataifa yote na watu wote kutekeleza maneno ya mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu ambao unatambua heshima ya asili na haki sawa kwa wote zisizoweza kukiukwa kwa watu wote duniani.”

Ameongeza kuwa ingawa hatua zinachukuliwa na wakiukaji wakubwa wa haki kukabiliwa na mkono wa sheria lakini bado kibarua kipo

Wafanya kazi wa MONUSCO wajiunga kuadhimisha siku ya kutokomeza ubaguzi wa rangi. Picha:
UN Photo/Abel Kavanagh
Wafanya kazi wa MONUSCO wajiunga kuadhimisha siku ya kutokomeza ubaguzi wa rangi. Picha:

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES

“Usawa wa kijinsia bado ni changamoto, pia tunashuhudia ongezeko la kutisha la chuki dhidi ya wageni, ubaguzi wa rangi na kutovumiliana ikiwemo chuki dhidi ya wayahudi na Waislam huku wakimbizi na wahamiaji wakinyimwa haki na kuonekana kama tishio kwa jamii wanakotaka kujiunga licha ya faina wanazozileta.”

Ametoa wito kwa dunia ikiadhimisha siku ya kotokomeza ubaguzi kufikiria njia za kuchagiza kuvumiliana, kujumuisha wote na kuheshimu utu na tofauto zetu katika mataifa yote na jamii zote duniani kwani jawabu pekee ni kuhubiri na kutekeleza kwa vitendo mambo haya, kuanacha na dhana ya “sisi na wao” na kukumbatia mchango wa kila mmoja.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter