Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyabiashara wa kigeni Afrika Kusini waripoti kuporwa kwa mali zao- UNHCR

Wajasiriamali Cape Town nchini Afrika Kusini
John Hogg/World Bank
Wajasiriamali Cape Town nchini Afrika Kusini

Wafanyabiashara wa kigeni Afrika Kusini waripoti kuporwa kwa mali zao- UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Kufuatia ongezeko la mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limeongeza msaada kwa wakimbizi lakini limetoa wito wa kuchukua hatua mara moja kukomesha mashambulizi hayo.

 Akizungumza na waandishi wa Habari hii leo mjini Geneva Uswisi,  msemaji wa UNHCR Charlie Yaxley amesema shirika hilo lina wasiwasi mkubwa kuhusu kujirudia kwa vitendo vya machafuko dhidi ya raia ya wakigeni wakiwemo wakimbizi na waomba hifadhi nchini Afrika Kusini na hivi karibuni machafuko hayo yalighubika eneo la Katlehong karibu na mji mkuu Johannesburg jimbo la Gauteng.

Bwana Yaxley amesema, “takriban watu 12 wakiwemo raia wa kigeni na wa Afrika Kusini wameripotiwa kuuawa tangu kuzuka kwa machafuko ya karibuni. Watu wapatao 1500 raia wa kigeni ambao asilimia kubwa ni waoomba hifadhi lakini pia wakimbizi wamelazimika kukimbia nyumba zao.”

Ameongeza kuwa siku za hivi karibuni wamekuwa wakipokea simu nyingi watu wakiripoti kwamba nyumba zao na biashara zao zimeporwa, majengo yao na mali zao kuteketezwa kwa moto, ongezeko la magenge ya uhalifu mitaani na kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na kingono .

Hivi sasa wakimbizi wengi wanaogopa kwenda kazini au kwenda kufanyabiashara zao za kila siku licha ya kutokuwa na mpango mbadala wa kujipatia kipato.

UNHCR imesema wakimbizi na waomba hifadhi wanahisi hatari zaidi kwani hali yao inaongezwa ugumu Zaidi kwa kutokuwa na nyaraka muhimu hali ambayo inawaacha wakihaha kupata huduma za afya , elimu, na huduma zingine za kijamii.

Takribani watu 800 wengi wakiwa kutoka Msumbiji, Malawi na Zimbabwe wanapatiwa hifadhi katika ukumbi wa jamii mjini Katlehong.

Kwa mujibu wa UNHCR wengi wa watu hao wanataka kurejea nyumbani kwani wanahisi usalama wao uko mashakani nchini Afrika Kusini.

Duru za Habari zinasema hadi sasa raia 73 wa Malawi, 138 wa Msumbiji, 314 wa Nigeria na 72 wa Zimbabwe wamesharejea nyumbani.

UNHCR inatoa wito kwa mamlaka ya Afrika Kusini kuchukua kila hatua zinazowezekana kuhakikisha ulinzi na usalama wa watu. Wafanye kila juhudi kuhakikisha wanakabiliana na machafuko na kurejesha utawala wa sharia na wahusika wa machafuko na ukatili huo lazima wawabjibishwe na mahakama.

Hivi karibuni serikali ya Afrika ya Kusini imepitisha mkakati wa kitaifa kukabiliana na ubaguzi wa rangi, kukomesha ubaguzi wa aina yoyote ile, chuki dhidi ya wageni na hali ya kutovumiliana mkakati ambao sasa unapaswa kutekelezwa ili kuepuka zahma zaidi na uharibifu mwingine.