Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chondechonde tushikamane na Brazil kuwasaidia Wavenezuela-Grandi

Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi, akizungumza na mama na mwanae kijiji cha Brasilia, Brazil
© UNHCR/Santiago Escobar-Jarami
Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi, akizungumza na mama na mwanae kijiji cha Brasilia, Brazil

Chondechonde tushikamane na Brazil kuwasaidia Wavenezuela-Grandi

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Filippo Grandi amehitimisha ziara ya siku nne nchini Brazil na kutoa wito wa haraka wa kuongeza ushirika wa kimataifa zikiwemo taasisi za fedha na wadau wa maendeleo katika jamii zinazowahifadhi wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela.

“Mshikmano wa watu wa Brazili kwa wahamiaji na wakimbizi wa Venezuela umekuwa ni mfano wa kuigwa.” Amesema Grandi lakini akiongeza kuwa athari kwa jamii zinazowahifadhi katika majimbo kama Roraima na Amazonas ni kubwa mno. “Nimeelezwa kwamba katika baadhi ya jamii za mpakani asilimia 40 ya wagonjwa na asilimia 80 ya wanawake wanaojifungua  katika hospitali wanatoka Venezuela. Kumekuwa na athari kama hizo pia katika elimu, ajira, makazi na huduma zakijamii.Ni muhimu kwamba juhudi zinazofanywa na serikali kuu, ya majimbo na hata ngazi za chini pamoja na asasi za kiraia, makundi ya makanisa na raia wa kawaida wa Brazili zikaungwa mkono na kupigwa jeki na jumuiya ya kimataifa. Watu wa maeneo hayo wamekuwa msitari wa mbele kusaidia katika mahitaji ya wakimbizi na wahamiaji toka Venezuela, hawapaswi kuachwa peke yao.”

UNHCR inasema kuna zaidi ya wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela 180,000 nchini Brazil, kwa wastani 500 wanawasili kila siku na wengi wao wakihitaji haraka msaada wa kibinadamu kwenye jimbo la Roraima Kaskazini Mashariki mwa Brazil jimbo ambalo kijiografia limejitenga na maeneo mengine ya nchi na lina kipato ch chini na fursa chache sana za kiuchumi.

Hatua zilizochukuliwa na Brazil

Kamishna Mkuu wa UNHCR wakati alikutana na watoto wakimbizi kutoka Venezuela akiwa ziarani Brazil.
© UNHCR/Santiago Escobar-Jarami
Kamishna Mkuu wa UNHCR wakati alikutana na watoto wakimbizi kutoka Venezuela akiwa ziarani Brazil.

Na katika juhudi za kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela serikali ya Brazili imezindua mpango wa  (Operacao Acolhida) unaoratibiwa na vikosi majeshi ya Brazil , ili kuwasaili na kuwapa nyaraka zinazohitajika watu hao piandi wanapowasili pamoja na msaada wa dharura wa kibinadamu ikiwemo chakula na malazi ya muda. Mwezi Aprili 2018 mpango mwingine ulizinduliwa ujulikanao kama  “Interiorizacao” kwa ushirikiano wa serikali, UNHCR , mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa , asasi za kiraia na sekta binafsi kwa lengo la kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji hao. Kwa mujibu wa Bwana Grandi hadi sasa wavenezuela 15,000 wamehamishwa kutoka Roraima kwenda katika miji mwingine 50 ambako kuna fursa zaidi ili kulipunguzia shinikizo jimbo hilo la mpakani.

“nimetiwa moyo sana na operesheni zote kama mfano wa kuigwa katika mafanikio ya uratibu , utu na ubunifu wa kushughulikia mahitaji ya kibinadamu na kuchagiza suluhu kwa Wavenezuela wanaokimbia. Hata hivyo changamoto bado zikokutokana na ongezeko la idadi ya wanaowasili kila siku. Katika iara yangu suala la muhimu lilitajwa kuhusu watu wa asili wa Venezuela, hali mbaya ya Wavenezuela wengi wanaoishi nje ya makazi rasmi na athari kwa miundombinu na huduma za kijamii kwa wenyeji. Hivyo hatua za haraka zinahitajika kutoka kwa serikali kuu, kwa msaada wa asasi za kiraia na mfumo wa Umoja wa Mataifa kushughulikia masuala ya afya, elimu, maisha na mahitaji mengine ya muhimu.”

Kabla ya kuwasili Brazil Grandi alipita Chile ambako ameishikuru serikali na watu wa nchi hiyo kwa juhudi walizozifanya za kupokea na kutoa msaada kwa wakimbizi na wahamiaji zaidi ya 400,000 jutoka Venezuela. Amesema idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji Zaidi ya milioni 4 kutoka Venezuela wamepokelewa na kusaidiwa katika nchi za Amerika ya Kusini.