Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa kuhamisha wakimbizi watoa matumaini mapya Brazil:UNHCR

Wakimbizi wa Venezuela wakiwasili Manaus, Brazil
César Nogueira/ Acnur Brasil
Wakimbizi wa Venezuela wakiwasili Manaus, Brazil

Mradi wa kuhamisha wakimbizi watoa matumaini mapya Brazil:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Mradi wa serikali ya Brazil na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR wa kuwahamisha wakimbizi umeleta matumaini mapya kwa maelfu ya wakimbizi wa Venezuela walioko mashambani nchini Brazil. Brenda Mbaitsa na taarifa Zaidi

Mradi huo unawahamisha kwa ndege maelfu ya Wavenezuela walioko katika maeneo ya mashambani ya jimbo la Amazon na kuwapeleka katika maeneo ya mijini kwa lengo la kusaka ajira bora na kuwasaidia kuanza upya maisha yao baada ya kukimbia madhila nchini mwao.

Kwa mujibu wa UNHCR zaidi ya wahamiaji na wakimbizi wa Venezuela 16,000 wameshiriki mradi huo hadi sasa ambao unaendeshwa kwa ushirikiano wa serikali, UNHCR na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM.

Shirika la UNHCR limekuwa likiongeza idadi ya malazi ambayo yanawapokea watu wanaohamishwa ili watu wengi zaidi waweze kutumia fursa ya mradi huo  kwa ajili yao na familia zao.

Mbali ya kuwasafirisha kwa ndege UNHCR pia imekuwa ikigawa fedha taslim kwa baadhi ya wakimbizi waweze kununua bidhaa za msingi na vifaa nyumbani katika miji mipya wanakohamishiwa.

 

Wahamiaji na wakimbizi hao wamekuwa wakihamishwa katika miji karibu 300 kote nchini Brazili na UNHCR inaamini kuwa huko wakimbizi na wahamiaji watapa fursa zaidi za ajira, kiuchumi, kielimu na kuweza kujikimu wao, familia zao na kupunguza mzigo kwa jamii zinazowahifadhi.

 

Takriban Wavenezuela 200,000 kati ya milioni 4.8 ambao wameikimbia nchi yao kufuatia mgogoro unaoendelea hivi sasa wamekimbilia na kupata hifadhi katika nchi jirani ya Brazil.